Na mwandishi wetu
Ubungo, 26 Julai 2025 – Hafla ya mahafali ya wafugaji wa kuku waliohitimu mafunzo ya ufugaji bora imefanyika leo katika wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, chini ya mradi ulioandaliwa na kampuni ya SAD Investment. Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mheshimiwa Albert Msando.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Wilaya alipongeza SAD Investment kwa kuanzisha mradi wenye tija unaolenga kuwajengea wananchi uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia ufugaji wa kuku. Alisema kuwa mradi huo ni mfano bora wa ubunifu wa sekta binafsi katika kusaidia juhudi za serikali kuinua kipato cha wananchi na kupunguza tatizo la ajira.
“Mradi huu si tu unatoa maarifa bali unawapa washiriki mbinu za kisasa za ufugaji, usimamizi wa biashara na kuongeza tija kwenye uzalishaji. Huu ni mfano wa miradi tunayotaka kuiona katika wilaya yetu,” alisema Msando.
Zaidi ya washiriki 100 walihitimu mafunzo hayo, wakikabidhiwa vyeti vyao vya kuhitimu katika hafla hiyo. Mafunzo yalijumuisha mbinu za utunzaji wa kuku wa kienyeji na wa kisasa, usalama wa chakula, afya ya mifugo, pamoja na mbinu za masoko na uendeshaji wa miradi ya biashara ndogondogo.
Mkurugenzi wa SAD Investment, Bi.Saida Bwanakheri alisema kuwa lengo la mradi ni kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi kwa kuwapatia elimu na vitendea kazi vya kuanzisha miradi ya ufugaji. Alieleza kuwa kampuni yao itaendelea kufuatilia maendeleo ya wahitimu na kuwapa msaada wa kitaalamu wanapoanza shughuli zao.
Wahitimu walielezea furaha yao kwa kupata ujuzi wa kuwasaidia kujiajiri na kusaidia familia zao. Baadhi yao walionesha kuku waliowafuga kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo na walitunukiwa zawadi kwa kuwa mfano bora wa utekelezaji wa mafunzo.
Mahafali hayo yalipambwa na burudani mbalimbali, maonyesho ya bidhaa za kuku, na kauli mbiu ya hafla ikiwa: "Ufugaji wa Kuku ni Ufunguo wa Maendeleo ya Uchumi wa Mtu Mmoja na Taifa Kwa Ujumla
0 Comments