Na.Mwandishi Wetu - Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza Watanzania katika Maadhimisho ya siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, inayotarajiwa kufanyika tarehe 25 Julai, 2025 katika Viwanja vya Mashujaa Mtumba Jijini Dodoma.
Akiongea na Waandishi wa Habari Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, amesema Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa ni tukio muhimu linalokumbusha dhamira, ujasiri na kujitolea kwa Watanzania waliotoa maisha yao kwa ajili ya Taifa, na ametoa wito kwa wananchi kuienzi siku hiyo kwa vitendo vya uzalendo na mshikamano wa kitaifa.
Dkt. Biteko amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ni fursa ya kipekee ya kutafakari mchango wa mashujaa waliolinda na kulijenga Taifa, na kuwahimiza Watanzania kuendelea kuithamini historia hiyo.
“Tunapoadhimisha Siku ya Mashujaa, tunawakumbuka wale waliopoteza maisha yao kwenye medani za vita, waliostaafu baada ya kulitumikia Taifa kwa uaminifu, na wale waliopata majeraha kwa ajili ya kulinda uhuru, amani na hadhi ya nchi yetu. Ni wajibu wetu kuenzi sadaka yao kwa vitendo vya uzalendo, mshikamano, na kujitolea kwa maendeleo ya Taifa,” alisema Dkt. Biteko.
Alifafanua kuwa sehemu ya maombolezo, Mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa utawashwa rasmi saa 6:00 usiku wa Julai 24, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule, kwa niaba ya Rais, kuashiria kuanza kwa siku ya heshima kwa mashujaa wa Taifa.
Maadhimisho hayo yataendelea Julai 25 kuanzia saa 3:00 asubuhi kwa gwaride rasmi la heshima kutoka Vikosi vya Ulinzi na Usalama. Mwenge wa Mashujaa utazimwa rasmi saa 6:00 usiku siku hiyo hiyo, kuhitimisha kumbukumbu za mwaka huu.
Dkt. Biteko ametoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye tukio hilo, akisisitiza kuwa ni siku ya kitaifa inayobeba historia, heshima na moyo wa uzalendo. Vilevile, amevitaka vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kushirikiana na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa Siku ya Mashujaa.
“Tuendelee kuwafundisha watoto wetu maana ya ushujaa, thamani ya kujitolea, na umuhimu wa kulipenda Taifa lao. Kwa kufanya hivyo, tunalinda msingi wa Taifa letu na kuendeleza kazi nzuri waliyotuachia mashujaa wetu,” alisisitiza
0 Comments