WAZIRI DKT. GWAJIMA- UWEZESHAJI WANAWAKE NA WASICHANA UNA MISINGI YA KATIBA YA NCHI.

 


 *New York, Marekani* 

------------------------------


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum *Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima* amesema, Tanzania imeweka misingi kwenye Katiba ya nchi kuhusu ajenda ya maendeleo yenye usawa wa kijinsia na mahsusi kuhusu Uwezeshaji Wanawake na Wasichana kupitia sekta mbalimbali. 

 *Dkt. Gwajima* ameyasema hayo Machi 12, 2025 wakati akichangia mjadala kwenye mkutano wa kimataifa unaohusisha Wajumbe wa nchi Jumuiya za Umoja wa Kimataifa kwa lengo la kujadili nafasi ya mwanamke katika nchi zao ikiwa ni miaka 30 baada ya maazimio ya Beijing.

 *Dkt. Gwajima* amesema chini ya Uongozi wa *Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan,* Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzbar *Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi* Sera, Mikakati na Sheria mbalimbali zimeendelea kuboreshwa Ili kuwagusa Wanawake na Wasichana zikiwemo Sera za Maendeleo ya Wanawake na Jinsia kwa Tanzania na Zanzbar. 

Aidha, kuna Sera ya Taifa ya Biashara inayohakikisha usawa wa kijinsia kwenye biashara, Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo inayohakikisha watoto wote bila kujali jinsia au umri wanahitimu elimu na mafunzo, pamoja na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa inayotaka mamlaka hizo kutenga 10% ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu. 

Vilevile, ameelezea uwepo wa Sheria ya Manunuzi ya Umma inayohakikisha asilimia 30 ya zabuni inawanufaisha Wanawake na Makundi Maalum jambo hilo  huwapa fursa Wanawake kupata tenda mbalimbali ambazo zinawasaidia kuongeza kipato binafsi, familia na taifa kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, *Dkt. Gwajima* amesema, Tanzania imefanya juhudi kuhakikisha takwimu za maendeleo zinakusanywa na zinafanyiwa uchambuzi wa kijinsia kwa ajili ya matumizi yenye kusukuma maendeleo yenye usawa wa kijinsia, na bajeti za kijinsia hatua ambayo ni muhimu katika kuhakikisha raslimali zilizopo zinatumika kusukuma masuala ya usawa wa kijinsia.

 *Dkt. Gwajima* ameweka wazi kwamba, Tanzania inaendelea kutekeleza mipango yote hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje.



Post a Comment

0 Comments