MITIHANI YA KIDATO CHA SITA KUANZIA 2,MEI 2023

 


Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dkt. Said Ally Mohamed akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza kuhusu kuanza kwa mitihani ya kidato cha sita pamoja na ualimu katika ngazi ya Stashahada na Cheti. Mitihani hiyo inatarajiwa kuanza Mei 2,2023 na kumalizika Mei 22, 2023

Na mwandishi wetu 

JUMLA ya watahiniwa 106,956 wamesajiliwa kuanza kufanya mitihani yao ya kumaliza kidato cha sita siku ya Jumanne,  Mei 2, 2023 hadi kumaliza Mei 22. 2023.

watahiniwa wa kidato cha sita 96,914 watafanya mitihani katika shule za sekondari 883 na watahiniwa 10,424  wa kujitegemea watafanya mitihani yao katika vituo 257.

Pia watahiniwa 8,906  kutoka vyuo 95 wamesajiliwa kufanya mitihani ya mwisho ya kozi ya ualimu katika ngazi ya stashahada na cheti kuanzia Mei 2,2023 na kumaliza Mei 16,2023.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, (Necta), Dkt. Said Ally Mohamed ameyasema hayo leo Aprili 30, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. 

"Kati ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa, wanaume ni 53,324 sawa na 55% na wanawake ni 43,590 sawa na 45% huku watahiniwa wenye mahitaji maalumu wakiwa ni 181 ambapo kati yao 114 ni wenye uoni hafifu, 14 ni wasioona, 28 wenye ulemavu wa viungo vya mwili na mmoja ni mwenye mtandio wa akili" amesema Dkt. Mohamed.

Amesema, kati ya watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa 10,041 wanaume ni 6,248 sawa na 62% na wanawake ni 3,793 sawa na 38% huku watahiniwa mwenye uoni hafifu akiwa ni mmoja.

Aidha kati ya walimu watakaoketi  kufanya mtihani huo, 2,344  ni ngazi ya stashahada na 6562 ni ngazi cheti. Ambapo kwa ngazi ya Stashahada wanaume ni 1438 sawa na 61% na wanawake 906 sawa na 39%.

" Watahiniwa 6,562 wa ngazi ya cheti, watahiniwa 2885 sawa na asilimia 44 ni wanaume na wanawake 3677 sawa na asilimia 56 huku wasioona wakiwa ni watatu kwa ngazi ya Stashahada na wanne kwa ngazi ya cheti  na mtahiniwa asiyeona kabisa akiwa ni mmoja" amesema

Dkt. Mohamed amesema baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajiridhisha kuwa kuna ukiukwaji wa taratibu za mitihani ambazo zinahatarisha usalama wa mitihani ya Taifa.

"Baraza linatumia nafasi hii kuwataka wamiliki wa shule wote kutambua kuwa shule ni vituo maalumu vya mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyaji mitihani hii," amesema Dkt. Mohamed. 

Post a Comment

0 Comments