RAIS MWINYI: SERIKALI KUENDELEZA JUHUDI ZA KUIFUNGUA PEMBA

 



Na mwandishi wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali kuendeleza juhudi za kuifungua Pemba kimaendeleo, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali inaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kuu na za vijijini, kutengeneza bandari za Mkoani, Shumba na kuanza matayarisho ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 2 Novemba 2024 katika viwanja vya Gombani, Mkoa wa Kaskazini Pemba, alipozindua Kampeni ya Kijana Kijani kwa upande wa Pemba ikiwa ni shamrashamra za kupongeza miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane, anayoiongoza.

Aidha , Rais Dk. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali, hadi kufikia mwezi Machi 2024, kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, tayari imetoa zaidi ya shilingi bilioni 31.8 kwa wajasiriamali wadogo wadogo Unguja na Pemba, ambapo asilimia 40 ya wanufaika ni vijana wa umri wa miaka 18-35.

Vilevile Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha eneo la uwekezaji la Micheweni na eneo la viwanda Chamanangwe kwa kuyawekea miundombinu, na kuongeza kuwa tayari kuna wawekezaji waliojitokeza kuwekeza katika maeneo hayo, hatua aliyoieleza kwamba itaongeza fursa za ajira kwa vijana.

Kampeni ya “Kijana Kijani” yenye kauli mbiu "Tunazima zote, tunawasha kijani" imefanikiwa kuingiza wanachama wapya 1,135 kutoka chama cha upinzani cha ACT Wazalendo na CUF, wakiwemo wanachama mashuhuri na viongozi waandamizi wa vyama hivyo.




















Post a Comment

0 Comments