WAFANYABIASHARA 6140 KIGOMA KUNUFAIKA NA UJENZI WA SOKO LA MWANGA NA KATONGA

 



Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amesema wafanyabiashara wa Manispaa ya Kigoma wapatao 4140 watanufaika na ujenzi wa Soko la Kisasa la Mwanga na wengine 2000 watanufaika na ujenzi wa Soko la Samaki Katonga, ambayo yanajengwa kupitia mradi wa TACTIC unaosimamiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Mhe. Katimba amesema hayo wakati akizungumza na wananchi kwenye Viwanja vya Mwanga Kigoma Ujiji, wakati wa hafla ya utiaji saini wa ujenzi wa Soko Kuu la Mwanga na Soko la Samaki Katonga katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma.

Akizungumzia ujenzi wa Soko la Kisasa la Mwanga, Mhe. Katimba amesema hapo awali Soko la Mwanga lilikuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 1246 lakini ujenzi wake utakapokamilika litakuwa ni soko la kisasa lenye uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 4140. 

“Mara baada ya ujenzi wa soko hili kukamilika, litakuwa na vizimba 1000, maduka 3040, litachukua mamalishe 100 na litakuwa na kituo cha polisi tofauti na lilivyokuwa hapo awali, hivyo maboresho ya soko hili yataongeza mapato ya Manispaa ya Kigoma kwa mwaka kutoka milioni 450 hadi bilioni 1.42,” Mhe. Katimba amefafanua.

Aidha, Mhe. Katimba amesema kuwa, ujenzi wa Soko la Samaki Katonga ukikamilika wafanyabiashara 2000 watanufaika, tofauti na hapo awali ambapo lilikuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 270.

“Ujenzi wa Soko la Samaki Katonga ukikamilika litakuwa na vizimba 300, maduka 800 na vyumba vya kutunzia samaki (cold room) 10 hivyo mapato ya Manispaa ya Kigoma kwa mwaka yataongezeka kutoka milioni 31 iliyokuwa inakusanywa hapo awali hadi milioni 183.2,” Mhe. Katimba amesisitiza.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Humprey Kanyenye amesema kuwa, mikataba ya ujenzi wa masoko hayo ya Mwanga na Katonga yaliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji ina thamani ya shilingi bilioni 16.49.

Mkandarasi aliyepewa kandarasi ya ujenzi wa masoko hayo mawili yanayojengwa kupitia mradi wa TACTIC anatakiwa kukamilisha ujenzi ndani ya miezi 12 na utekelezaji wake unaanza rasmi Novemba 15, 2024.










Post a Comment

0 Comments