Na Saidi Lufune – Nantumbo, Songea
Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba amesema Serikali itaendelea kukipa thamani chuo cha Likuyu Sekamaganga kutoa mafunzo ya uhifadhi wa maliasili ya jamii ili kushiriki kikamilifu katika shughuli za utalii na matumizi endelevu ya rasilimali za Taifa.
CP. Wakulyamba amesema hayo katika Mahafali ya nne (4) ya Mafunzo ya kozi ya utalii na uongozaji watalii kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada ambapo amesema uwepo wa chuo hicho ni fursa muhimu kwa watanzania katika kupata ujuzi na maarifa ya kulinda na kuhifadhi urithi wa Taifa na kuongoza watalii kwenye vivutio vya utalii
’’Chuo hiki kimekuwa nguzo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutoa elimu ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) ambao wamekuwa msaada mkubwa katika kukabiliana nao” Amesema Wakulymba
Katika hatua nyingine CP. Wakulymba amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kufanya kazi kwa weledi uadilifu na ukarimu ili kua mabalozi wazuri katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania na kuenzi kwa vitendo maono ya Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii hususani kupitia filamu ndani na nje ya nchi
‘‘Sekta ya Utalii huchangia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira kwa takriban milioni moja la laki sita kila mwaka na kuchangia uchumi wa nchi hii kwa asilimia 17 ya pato la Taifa na asilimia 25 kwa fedha za kigeni, hivyo tumieni ujuzi mliopata hapa kama fursa ya kujikwamua kiuchumi badala ya kusubiri serikali iwaletee ajira” Amesema Wakulyamba
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo Bi. Kanisia Mwadua ameshukuru Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) , Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) , Makumbusho ya Taifa na Halmashauri za Wilaya kuendelea kushirikiana na chuo hicho kutoa maeneo ya kupatiwa mafunzo kwa vitendo
‘‘Imani yangu ushirikiano huu utakuwa endelevu kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa hamkisaidii chuo pekee bali Sekta nzima ya Utalii na Taifa kwa ujumla’’. Amesema Kanisia
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Bi. Jane Nyau ameishukuru Wizara hiyo kuendelea kukiwezesha chuo hicho kwa kuelekeza fedha kupitia bajeti ya kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kuboreha miundombinu ya chuo ikiwemo kuwekwa umeme wa grid ya Taifa, nishati mbadala ya gesi, ujenzi wa madarasa, mabweni na kuongeza watumishi
“Uwezeshaji huu sio tu umekisaidia chuo kupunguza changamoto zake, bali pia utakisaidia kuboresha utendaji kazi kwa watumishi na kuongeza udahili pamoja na kuongeza mapato ya chuo, hivyo naomba Wizara iendelee kukiangalia chuo hiki kwa jicho la kipekee.’’ Amesema Jane
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo walionufaika kupitia mradi wa REGROW wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kutimiza ndoto zao za muda mrefu kwa kuwaongeza ujuzi na maarifa makubwa ikiwemo ukakamavu, kuongoza utalii na kukabiliana na ujagili
Jumla ya wahitimu 70 wamedahiliwa kwa mwaka wa masomo 2023/2024 kati yao 64 ni wahitimu wa ngazi ya Astashahada wakiume wakiwa 43 na wakike 21 huku wahitimu sita wa Stashahada wanaume wakiwa watatu na wanawake watatu ikijumuisha wanafunzi 34 waliofadhiliwa kupitia mradi wa REGROW na 36 wakitokana na ufadhili binafsi
0 Comments