BASHUNGWA ATOA MAAGIZO KWA IGP WAMBURA KUELEKWA SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA.

 


Na mwandishi wetu

📌 Kuimarisha ulinzi, doria na ukaguzi vyombo vya moto usiku na mchana.

📌  Kuondoa vizuizi na vituo vya ukaguzi maeneo hatarishi barabarani.

📌 Kufanya Operesheni maalum nchi nzima kupambana na wahujumu miundombinu ya Serikali

📌 Awahakikishia Watanzania nchi ipo salama.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa  amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura kulisimamia Jeshi la hilo kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto barabarani, kuimarisha doria (highway patrol) usiku na mchana pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye Nyumba za Ibada katika kipindi cha sikukuu za Christmass na Mwaka Mpya.

Bashungwa ametoa maagizo hayo, leo tarehe 18 Disemba 2024 wakati akitoa taarifa kwa Umma kuelekea Sikukuu za Mwisho wa Mwaka ambapo amewahakikishia wananchi na Watanzania wote kuwa nchi  iko salama.

“Hatuko tayari kuacha tabia za kizembe ziendelee kupoteza maisha ya watu, na wengine kupata ulemavu, huku Sheria za kudhibiti uzembe zikiwa zipo. Tutachukua hatua kali kwa madereva na wasafarishaji wazembe. Ninaomba wasafiri mtupe ushirikiano, na kuunga mkono jitihada hizi, ili tuwe salama tunapokuwa barabarani”amesema Bashungwa

Bashungwa ametoa wito kwa wasafiri na wasafirishaji, kuzingatia na kuheshimu Sheria za Usalama Barabarani, ili kupunguza ajali zinazoepukika ambazo zimekuwa zikisababisha vifo, majeruhi na hata kusababisha ulemavu kwa wananchi.

“Nitoe tahadhari kwa familia zinazotumia magari yao binafsi, kufanya matengenezo ya magari kabla ya safari, na kuacha utamaduni wa kuchukua mtu yeyote ambaye hana taaluma ya udereva, wala leseni, na hajapitia mafunzo ya kuendesha magari kwa kukwepa gharama. Kila familia ichukue tahadhari, hususani tunapoelekea mwisho wa mwaka.”

Aidha, Bashungwa ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana  na TANROAD pamoja na TARURA kukagua maeneo yote nchini yenye vizuizi na vituo vya ukaguzi, kuangalia kama vimewekwa kwa kuzingatia sheria, na tahadhari ya usalama kwa watumiaji wengine wa barabara na kama vipo katika maeneo hatarishi viondolewe.

“Pale itakapokutwa vizuizi ama vituo vya ukaguzi vimewekwa bila kuzingatia taaluma na uzingatiaji usalama wa watumiaji wengine wa barabara, wakutane na Taasisi au Mamlaka husika ili kuviondoa katika maeneo hatarishi, na kwa pamoja kukubaliana maeneo sahihi ya kuweka vituo hivyo” amesisitiza Bashungwa.

Kadhalika, Bashungwa amemuagiza IGP Camillus Wambura na Jeshi la Polisi kwa ujumla kuendelea na operesheni Maalum  katika mikoa yote nchini ya kupambana na wezi na wahujumu wamiundombinu ya TANESCO, SGR, barabara na miundombinu mingine na watuhumiwa wanaokamatwa, upelelezi ukamilike mapema na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kubwa katika maeneo yenye mikondo ya maji inayokatiza barabarani pamoja na wazazi na walezi kutoacha watoto kuvuka pekee yao kwenye maeneo hatarishi ya maji au kuogelea kwenye madimbwi kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo nchini.

“Upo utamaduni kwenye sherehe za mwisho wa mwaka, wazazi kuwaacha watoto kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea sikukuu, yakiwemo maeneo ya ufukweni au kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo ya watoto, huku wakiwa peke yao. Niwaombe wazazi kuwalinda watoto na kutoruhusu watoto kwenda kutembea siku za sikukuu wakiwa peke yao” amesisitiza

Pia, Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuipa ushirikiano Serikali ili kuifanya nchi kuendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu, na kuwafanya wananchi  kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Post a Comment

0 Comments