WAZIRI MKUU:SERIKALI IMESAJILI MIRADI YA UWEKEZAJI 537.

 


NA MWANDISHI WETU 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Januari, 2023 Serikali ilisajili jumla ya miradi ya uwekezaji 537 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 7,222.
 
Amesema hayo leo Alhamisi (Aprili 20, 2023) alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki, kinachojengwa na Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center kwenye eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa, hatua hiyo imetokana na kuboreshwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kuimarisha Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja ili kuvutia wawekezaji kwa kupunguza kero na kurahisisha utoaji huduma.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa ongezeko la usajili wa miradi hiyo unatarajia kutoa  ajira takriban 92,770 “Kiwango hiki ni kikubwa kuwahi kuandikishwa katika kipindi chochote tangu nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961”

Amesema kuwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Mauzo ya Nje (EPZA)  imefanikiwa kusajili Miradi 38 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 139.70 na mauzo nje yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 191.04.

“Miradi hiyo ni mahsusi katika sekta zinazozalisha bidhaa zitokanazo na Kilimo, bidhaa za viwandani, bidhaa za Mifugo, bidhaa za Kemikali, bidhaa za madini na bidhaa za misitu”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania kwani ni sehemu sahihi ya uwekezaji, na  kuleta mitaji yao “tunayo mazingira mazuri ya uwekezaji”

Akizungumzia kuhusu Mradi wa Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kituo hicho kitakuwa na maduka zaidi ya elfu mbili, ambayo yatakuwa na ukubwa tofauti tofauti hivyo kuweza kukidhi mahitaji ya wafanyabishara wa aina tofauti tofauti “Kutokana na ukweli huo, mtakubaliana nami kuwa kituo hiki kitapanua fursa ya Watanzania wengi kufanyabiashara katika eneo hili”.

Amesema kuwa kituo hicho pia kitatoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo almaarufu Wamachinga kufanya biashara zao katika eneo la nje baada ya kusitisha shughuli za kituo hiki kila siku

“Kitendo hiki ni cha kizalendo kwani kitatoa fursa kwa Watanzania wenye kipato cha chini ambao hawatakuwa na uwezo wa kupata vizimba ndani kunufaika na uwepo wa kituo hiki kwa kuweka biashara zao nje kwa muda watakaopangiwa”.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Angellah Kairuki amesema kuwa mradi huo unathamani ya dola za Kimarekani milioni 81.827.

Amesema kuwa Mradi huo utaifungua Tanzania kibiashara na kukuza uchumi kutokana na biashara zitakazokuwa zikifanyika na kukuza mahusiano ya Kimataifa kwa kuwa na muingiliano wa wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali.

Ameongeza kuwa kituo hicho kitatoa ajira za moja kwa moja zaidi 15000 na utahamasisha maendeleo ya setka mbali mbali ambazo nazo zitazalisha ajira zisizo za moja kwa moja 50000 hivyo kuongeza mapato na kuboresha hali ya maisha kwa wananchi wa Tanzania.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC) Dkt. Cathy Wang amesema kuwa mapato ya jumla kwa mwaka yatafika zaidi ya dola za marekani milioni 500 pindi mradi huo utakapokamilika hivyo kusaidia katika ukuaji wa pato la taifa na kuongeza mapato ya kikodi.

Amesema kampuni hiyo imedhamiria kujenga mradi huo wa kimkakati ambao utakuwa moja ya mradi mkubwa ndani ya afrika mashariki na utawezesha kukuza biashara ndogo nchini na kupanua biashara hizo ndani ya soko kubwa la Afrika.

Amesema kuwa mradi huo utasaidia kukuza biashara ndogo na kupanuka zaidi ndani ya soko la afrika na utawezesha kuchachusha ukuaji wa uchumi endelevu ifikapo 2025.

Mradi huo utakuwa na maduka 2060 yenye ukubwa wa jumla ya mita za mraba 75000 ambapo eneo hilo litakuwa na huduma zote za kibiashara ikiwemo mabenki na huduma ufungishaji na usafirishaji.
 
Pia, Mapato ya jumla kwa mwaka yatafikia zaidi ya USD Milioni 500 mradi huo ukiwa umekamilika hivyo kusaidia katika ukuaji wa pato la Taifa la Tanzania na kuongeza mapato ya kikodi.



Post a Comment

0 Comments