AJALI ZAPUNGUA KWA ASILIMIA 61

 




Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP. Ramadhani Ng’anzi amesema katika kipindi cha miezi mitatu, kutoka Januari hadi Machi 2023 ajali za barabarani zimepungua kwa kiasi kikubwa kwa asilimia 61% huku akibainisha kuwa vifo vinavyotokana na ajali hizo vimepungua kwa asilimia 8% tofauti na mwaka uliopita.


SACP Ramadhani Ng’anzi amesema hayo, Aprili 30, 2023 jijini Dar es Salaam akiwa sanjari na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) katika kikao cha pamoja na Waandishi wa Habari.


“Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani tunafanya uhakiki wa Shule na Vyuo vinavyotoa mafunzo ya Udereva, zoezi hili limekuja baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuvunja Dawati la Utoaji Leseni za Udereva.”


“Kwa sababu tuliamini chanzo kimoja wapo cha ajali ni Madereva kutokuwa mahiri na kukosa ustadi pindi wawapo barabarani, yote ilisababishwa na mfumo wa utoaji Leseni kuwa mbaya, Dawati lilivunjwa na kuundwa upya,” ameeleza SACP. Ng’anzi


SACP. Ng’anzi amesema ili kupunguza ajali hizo, kuanzia Januari 2 mwaka huu walianza kuchunguza na kuhakiki Shule za Udereva, ambapo jumla ya Shule 297 zilihakikiwa na kukaguliwa, amesema Shule 134 zilikuwa na sifa huku Shule 161 zikikosa sifa na vigezo mbalimbali katika usimamizi na uendeshaji wake na kufungiwa.


“Sifa za Vyuo vya Mafunzo ya Udereva zinatakiwa kuwa na vigezo vya Leseni kutoka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Wakufunzi wenye Weledi wa kutosha, Magari mazima na yenye hadhi ya kujifunzia, Madarasa yanayofaa na Mitaala rasmi ya mafunzo ya Udereva,” amesema SACP. Ng’anzi


Aidha, SACP. Ng’anzi amesema uhakiki wa hiari wa Leseni za Udereva hadi sasa Madereva 20,944 tayari wamehakiki Leseni zao kwa Madaraja C na E ikiwa sawa na asilimia 2% tu ya Madereva, wakati katika idadi hiyo Leseni 17,726 zimethibitishwa kuwa sifa na Leseni 3,214 zimekosa sifa ya kuwa na Maderaja C na E kuendesha Mabasi na Malori.


Post a Comment

0 Comments