Na Mwandishi Wetu,Same
MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeniameendelea na ziara zake za kusikiiza kero na malalamiko ya wananchi ambapo akiwa Kata ya Kihurio amepata fursa ya kutembelea mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Uzambala ambao umetengewa Sh.milioni 247 kwa ajili ya kufanya matengenezo.
Wananchi wa eneo hilo walimueleza Mkuu wa Wilaya Kasilda kwamba moja ya changamoto kubwa inayowakabili na uhaba wa Maji,hivyo kabla ya kufanya mkutano wa hadhara akaamua kuitembelea mradi huo . Wananchi walitaka kufahamu hatma ya mradi huo.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ,wananchi walimueleza kuwa Waziri wa Maji Juma Awezo alipofika kukagua mradi huo Julai mwaka 2021 aliagiza ukarabati ufanyike ndani ya miezi 3 uwe umekamilika ili wapate huduma ya maji , lakini mpaka sasa hawajui kinachoendelea kwani tatizo la maji liko pale.
Kutokana na malalamiko hayo Kasilda alimtaka Meneja wa RUWASA Wilaya ya Same kutoka maelezo kuhusiana na mradi huo ambapo alieleza mradi wa maji ulishakarabatiwa na fedha ilishakwisha Hata hivyo maji yameshindwa kutoka kutokana na ukarabati huo kutokuwa na matokeo mazuri kwani mradi huo ni wasiku nyingi.
Meneja huyo alifafanua na miundombinu yake ilikuwa imekufa na ndiyo naana hata walipokarabati baadhi ya miundombinu yake haikusaidia na tatizo la maji bado ni kubwa kijiji hapo. Majibu ambayo wananchi hawakukubaliana nayo na kuhoji zilipokwenda sh.milioni 247.
Akizungumza baada ya maelezo ya Meneja wa RUWASA ,Kasilda amewaomba wananchi wawe watulivu na kuwahakikishia atatumia vyombo vyake kwenda kijiji hapo kuchunguza ili kupata ukweli kuhusu fedha zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati wa mradi huo.
Aidha amewataka Meneja wa Bodi ya Maji na Mhasibu wake kujitadhimini katika utendaji wao kwa kuwa wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi kutokana na kutotaka kutoa majibu yeyote kuhusu mradi huo,hivyo wananchi kukosa imani nao.
Pia amewataka kunapotokea mabadiliko yeyote katika sekta ya maji ikiwemo kupanda kwa bili za maji kutoka Sh. 2000 hadi Sh. 5000 kwa mwezi ambayo pia wananchi hawakuwa na uelewa kuhusiana na ongezeko hilo.
"Ni vema mkatumia vikao vya kisheria vya bodi ya maji kutoa ufafanuzi kwa wananchi badala ya kunyamaza na kuzua masuala mengi toka kwa wananchi,"amesema huku akimtaka Meneja wa RUWASA wilayani ambaye ni mgeni kuhakikisha anawasimamia maofisa wake wa bodi ya maji na kuchukua hatua pale anapoona hawawajibiki .
0 Comments