JESHI LA POLISI DAR LAPIGA MARUFUKU MTU ASIYE NA TIKETI KUSOGELEA UWANJA WA BENJAMINI MKAPA MECHI YA SIMBA NA AL AHLY

 


Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku mtu asiye  na tiketi kusogelea Uwanja wa Benjamin Mkapa au maeneo ya milango ya kuingia ili usalama uimarishwe zaidi siku ya uzinduzi mashindano “African football league” ambapo  pia kutakuwa na mchezo wa soka hatua ya robo fainali ya mashindano baina klabu ya Simba ya Tanzania na Al Ahly ya nchini Misri utakaochezwa kuanzia saa 12:00 jioni.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 18, 2023 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatambua kuwa Ijumaa, Oktoba 20, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es Salaam kutakuwa na uzinduzi mashindano “African football league” ambapo  pia kutakuwa na mchezo wa soka hatua ya robo fainali ya mashindano hayo baina klabu ya Simba ya Tanzania na Al Ahly ya nchini Misri utakaochezwa kuanzia saa 12:00 jioni,” amesema SACP Muliro na kuongeza,

“Pia Jeshi la Polisi linatambua mchezo huo utahusisha wageni kutoka nje ya nchi na kuwa na mkusanyiko mkubwa katika Kiwanja hicho, kwa kulitambua hilo baadhi ya barabara zitafungwa ili kupunguza msongamano wa kuelekea uwanjani hapo, hivyo mashabiki wa soka wafike mapema ili kuepusba usumbufu unaoweza kuepukika,”.

Hivyo SACP Muliro amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limechukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo huo kwamba ukaguzi wa hali ya juu katika mageti ya kuingia na  haitaruhisiwa mtu yeyote kwenda uwanjani na silaha ya aina yoyote, isipokuwa baadhi ya vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo.

Aiddha amewatahadharisha baadhi ya mashabiki wenye tabia ya kuwasha fataki au baruti uwanjani, hayo ni baadhi ya makosa ya mambo ya kiusalama kwenye viwanja vya soka.

Kwamba Jeshi la Polisi halitavumilia tabia hizo na zingine ambazo zimepigwa marufuku  na  vyama vya soka FIFA, CAF na TFF tabia ambazo zinaweza kupelekea Tanzania kukosa sifa ya kuandaa mashindano kama haya wakati mwingine.

Amesema watakao kaidi, watakamatwa  na kuchukuliwa hatua za kisheria. Jeshi la Polisi linawatakia mashabiki wa soka kushangilia kistaarabu.

Post a Comment

0 Comments