TFRA yapongezwa kutembelea wadau kujua changamoto zao

 


Na mwanahabari wetu

Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imepongezwa kwa hatua ya kuwatembelea wadau katika ngazi mbalimbali, kusikiliza na kutafutia suluhu changamoto wanazokutana nazo katika tasnia ya mbolea. 

Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na viongozi wa Serikali, mawakala wa mbolea na wakulima pindi walipokutana na wajumbe wa Bodi hiyo kwa nyakati tofauti ndani ya Mkoa wa Rukwa.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika ofisini kwake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Donatus Wegina, amesema hatua hiyo ni muhimu sana katika kutatua changamoto za wakulima kutokana na kufika hadi ngazi za chini kuchukua maoni yao.

Amesema, Mkoa wake haukupata changamoto kubwa kwa msimu wa kilimo uliopita kutokana na jitihada walizozichukua za kutafuta magari ya Serikali na kampuni binafsi na mafuta ambapo hata TFRA walichangia na kuwezesha mbolea kuwafikia wakulima mpaka vijijini na kukiri uamuzi huo ulipunguza changamoto iliyotokana na uchache wa mawakala.

 Naye Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Lazaro Komba, ametoa pongezi nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua aina ya rasilimali zilizopo kwa wingi nchini na kuamua kuwekeza kwenye fikra za vijana na kuwafanya kukichukulia kilimo kama biashara.

"Zaidi ya asilimia 75 ya watanzania wanategemea kilimo kama ajira, na nchi yetu imejaaliwa kuwa na ardhi ya kutosha na inayofaa kwa kilimo, aidha nguvu kazi ipo,
Mhe. Rais anaelekeza maisha ya vijana kufikiri zaidi kwenye hiki tulichonacho ambacho ni kilimo" Komba alisisitiza.

Ameiomba TFRA kuendelea kuwasaidia ili kuhakikisha pembejeo sahihi za kilimo zinapatikana kwa wakati na kuwasaidia wakulima kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija kwenye kilimo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka, Dkt. Anthony Diallo amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza, kusikiliza changamoto na kupokea ushauri wa kuboresha tasnia ya mbolea nchini kutokana na bodi hiyo kuteuliwa muda mfupi uliopita.

Aidha, ameziomba Halmashauri na wadau wengine kushirikiana katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo, mbolea ikiwemo ili wakulima waongeze tija kwenye uzalishaji na kuonesha tija kwa juhudi na nguvu kubwa iliyofanywa na serikali katika kuinua kilimo. 

Amewataka maafisa ugani kutumia vifaa walivyopewa na Serikali kuwasaidia wakulima kutambua virutubisho vya mimea vinavyohitajika katika ardhi zao ili waweze kutumia mbolea sahihi.

Bodi hiyo imefanikiwa kuzungumza na viongozi wa Serikali kwa ngazi ya mkoa na wilaya, mawakala wa mbolea pamoja na chama cha ushirika cha msingi cha Mbara kilichofanikiwa kuanza kuuza mbolea kwa wakulima wa Laela Mkoani Rukwa.

Post a Comment

0 Comments