Waziri Mkuu Kivuli wa Chama cha ACT Wazalendo Isihaka Mchinjita akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema kuwa matukio ya maafa na majanga kwa miaka ya hivi karibu yameonyesha uwezo mdogo wa Serikali na kukosekana kwa utaratibu mzuri na kushindwa kuchukua tahadhari, kukabiliana na majanga mbalimbali nchini kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 8, 2024 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kivuli wa Chama hicho Isihaka Mchinjita akiwasilisha kwa waandishi wa habari Uchambuzi wa Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu Bajeti na Mwelekeo wa Serikali 2024/25.
"Mathalani tumeona Ofisi ya Waziri Mkuu ilivyoshindwa kabisa kuandaa utaratibu wa kukabiliana na dharura, matukio ya ajali zinazohitaji uokozi, kama vile kuungua kwa masoko ya wafanyabiashara hapa nchin, ajali za moto, ajali za uokozi kwenye vyombo vya usafiri (ndege, treni). Ukarabati na matengenezo ya miundombinu baada ya maafa kama vile mafuriko, tetemeko na ajali za moto," amesema Mchinjita na kuongeza,
"Mfano mwingine ni kuwepo kwa malalamiko ya kupunjwa na kutolipwa fidia wahanga (1361) wa mabomu ya Mbagala tangu mwaka 2009. Hata hivyo, ni jambo la kusikitisha kuona licha ya kunyimwa kucheleweshewa kwa haki zao wamekuwa wakipokea majibu ya kukatisha tamaa, kejeli na vitisho toka kwa watumishi wa Serikali ikiwemo watumishi toka Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa,".
Hivyo Mchinjita ametoa rai kwa Waziri Mkuu kuhakikisha mwaka huu wanafuatilia suala hili na kuwafuta machozi wahanga hao kwa kuwalipa fidia ya haki na kueleza kuwa tangu mwishoni mwa mwaka 2023 hadi sasa wameona udhaifu mkubwa wa kitengo cha maafa katika kuchukua hatua za dharura.
Kwamba Nchi ilitabiriwa kupokea mvua kubwa lakini Watanzania hawakuona hatua madhubuti zikichukuliwa kujiandaa na kujilinda na janga hili ili kuepusha au kupunguza athari zinazowapata wananchi sasa.
"Tulishuhudia maafa ya mafuriko kule Kateshi Hanang, wananchi wengi wamekufa, wamepoteza Makazi, Miundombinu imeharibiwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.Muda huu tunapozungumza Kijiji cha Taweta Kilombero mawasiliano bado hayajarudi, hakuingiliki wala hakutokeki, kumejaa maji, zaidi ya watu elfu moja wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu," amesema Mchinjita na kueleza,
"Vilevile ukanda wa Kibiti na Rufiji eneo linalozunguka Bonde la Mto Rufiji hasa lililopo karibu na Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere kuna hali mbaya sana, zaidi ya kata 12 zimeathirika vibaya na maji, mazao, makazi, huduma za msingi za kijamii vimeharibiwa vibaya, wananchi wengi wamejihifadhi kwenye shule ambazo hazijapatwa na maji. Hali ni mbaya sana,".
Hivyo ACT Wazalendo imemtaka Waziri Mkuu kufika Rufiji na Kibiti kuona hali halisi na kuhakikisha hatua za uhakika za haraka zinachukuliwa kwa wananchi wa maeneo hayo ambayo kwa sasa ni hatarishi na walipwe fidia.
Kadhalika afike pia Mlimba kwa ajili ya kujionea halihalisi na kuchukua hatua stahiki kwamba kwenye hotuba, hawajaona hatua za makusudi za kujenga uwezo wa kibajeti kununua vifaa vya kisasa vya uokoaji, kujenga uwezo wa idara ya maafa na taasisi zilizo chini yake.
Aidha wameitaka Serikali kutenga bajeti (fedha) ya kutosha ili kujenga uwezo wa idara ya maafa na kuongeza ufanisi wa usimamizi wa idara hiyo.
Amesema pia ni muhimu kujenga uwezo kwa kutumia teknolojia juu ya kufuatilia maafa sehemu mbalimbali za nchi na pia ameitaka Serikali kuchukua hatua za tahadhari kukinga majanga yanayoweza kujitokeza na kwa kuwa na mpango wa kabla wa kukabiliana na majanga (Proactive disaster management) badala ya kusubiri majanga yatokee ndio wasogee.
0 Comments