DKT MPANGO ATOA WITO KWA WATANZANIA WOTE KUONGEZA JITIHADA KUFAHAMU HISTORIA YA NCHI

 




Na mwandishi wetu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito watanzania wote hususani vijana kuongeza jitihada katika kufahamu historia ya nchi ili kuhakikisha wanapata uelewa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifanya mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuhusu Miaka 60 ya Muungano, mazungumzo yaliyofanyika katika Makazi ya Makamu wa Rais Jijini Dodoma. Amesema ni muhimu vijana kujifunza kupitia nyaraka, vitabu na kutambua historia ya Muungano na namna serikali zilivyofanya utatuzi wa changamoto mbalimbali kuhakikisha Muungano unadumu.
 
Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kuhusu Muungano kuanzia ngazi ya shule za msingi. Aidha amesema ni vema kutumia mbinu mbalimbali zinazoendana na vijana katika kutoa elimu hiyo ikiwemo Sanaa kama vile muziki na mitandao ya kijamii kujadili namna ya kujenga na kuimarisha Muungano kwa kujadili kwa hoja bila jazba.
 
Makamu wa Rais amesema katika kipindi cha Miaka 60 ya Muungano, mafanikio makubwa yamepatikana ikiwemo kuimarika kwa ulinzi na usalama, maendeleo ya kiuchumi, kukuza tamaduni na lugha ya Kiswahili pamoja na maendeleo ya kisiasa. Ameongeza kwamba ni Muungano wa kipekee zaidi duniani ambao umedumu kwa miaka 60.
 
Aidha amesema uwepo wa sera ya fedha ya pamoja na kuwa na usimamizi wa pamoja wa Benki Kuu ya Tanzania kumesaidia katika kuimarisha uchumi pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei kwa pande zote za Muungano. Makamu wa Rais amesema kukua kwa uwekezaji nchini ni kutokana na ukubwa wa soko lililopo linalochagizwa na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
 
Halikdahalika,Makamu wa Rais serikali zote mbili zinaendelea kuzipatia ufumbuzi hoja 4 za Muungano zilizobakia kutoka 25 za awali. Ametaja hoja zinazotafutiwa ufumbuzi ni pamoja na Suala la Sukari, Usajili wa Vyombo vya Moto, Bodi ya Pamoja na Mgawanyo wa Mapato ya iliyokuwa Sarafu ya pamoja ya Afrika Mashariki.
 
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewasisitiza watanzania kuongeza jitihada katika kulinda mazingira kwa kuchukua hatua za makusudi katika kupanda miti ikiwemo kila kaya kupanda miti mitatu. Amezitaka Halmashauri za Miji na Majiji kufanya jitihada katika kuanzisha bustani za kijani tatu ikiwemo bustani za mimea inayotoweka (Botanical Garden) na bustani kwaajili ya mapumziko na mazoezi kwa wananchi.
 
Makamu wa Rais ametoa wito kwa wadau kushirikiana na serikali katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuokoa misitu pamoja na kulinda afya za wananchi.
 
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
19 Aprili 2024
Dodoma.

Post a Comment

0 Comments