OR-TAMISEMI, Mara
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.Kanali Evans Alfred Mtambi amefunga mafunzo ya Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata mkoani humo na kuwataka kwenda kutatua kero za wananchi kwenye maeneo yao.
Mhe. Mtambi ameyasema hayo tarehe 25 Aprili, 2024 katika ukumbi wa Uwekezaji wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wa Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amesema ni wakati sasa kwa viongozi hao kwenda kutatua kero na malalamiko ya wananchi kwa kusaidia kutambua mahitaji na mategemeo halisi ya wananchi katika maeneo yao pamoja na kuchukua hatua stahiki kwa wakati na kama kero hiyo hawaiwezi basi waipeleke kwa viongozi wa ngazi ya juu ili kuleta ufanisi.
Mhe. Kanali Mtambi amewataka pia kusimamia miradi ya maendeleo kwa weledi kwani Serikali inatoa fedha nyingi na wao kama wasimamizi ni lazima kuhakikisha kuwa fedha za miradi zinatumika kufanya kazi zilizokusudiwa, kujua mahali inapojengwa na kwa thamani halisi ya fedha na si vinginevyo.
Katika hatua nyingine amewataka kukemea masuala ya kilimo cha mihadarati kama vile bangi, mirungi na mazao mengine kama hayo kwani yanaleta madhara makubwa kwa jamii.
Maagizo mengine ni pamoja na kuhamasisha wananchi kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 ili wajiandikishe kwa wingi na kuchagua viongozi wanaowataka ili kuepuka kuchagua viongozi wabovu ambao wataipelekea hasara Serikali hususani kwenye utekelezaji wa miradi na kufuja fedha za Serikali.
Kwa upande wake Ibrahim Minja Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema jumla ya Maafisa Tarafa 300 na Watendaji wa Kata 2,260 waliopo kwenye mikoa 16 tayari wamepata mafunzo ambapo lengo la Ofisi ya Rais TAMISEMI ni kuwapatia mafunzo viongozi hao kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na matarajio ni kuwa watumishi hao watarudi vituoni mwao wakiwa bora na kuimarika tayari kwa kufanya kazi zao kwa ufanisi.
0 Comments