Na mwandishi wetu
●Ujenzi wa Jengo wafikia asilimia 84.4
*Dodoma*
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt.Mathayo Mathayo amepongeza maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Madini awamu ya pili kwa juhudi mbalimbali zinazofanyika na kupelekea kufikisha asilimia 84.4 ya ujenzi katika mji wa Serikali Mtumba.
Dkt. Mathayo ametoa pongezi hizo leo Agosti 12 , 2025 jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mradi huo awamu ya pili linaloendelea kujengwa katika wa Mji wa Serikali Mtumba.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mkurugenzi wa Utawala na RasilimaliWatu, Festus Mbwilo amesema mpaka kufikia Agosti 2, 2024 utekelezaji wa ujenzi wa jengo hilo la ghorofa tano ulifikia asilimia 84.4 na sehemu iliyobakia ni asilimia 15.6.
Awali, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa utekelezaji wa mkataba ulikuwa miezi 18 lakini kutokana na changamoto mbalimbali mkandarasi hakuweza kukamilisha kwa wakati ambapo tarehe ya mkataba ya awali kukamilisha jengo ilikuwa Aprili 14, 2023.
Akielezea kuhusu changamoto zinazojitokeza katika ujenzi Mkurugenzi wa Sera na Mipango wizara ya madini Augustine Ollal amesema kumekuwepo na mabadiliko ya mifumo hususani mifumo ya zimamoto ambayo inapelekea mkandarasi kusubiri maelekezo yanayojumuisha wizara zote kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ili kukamilisha ujenzi.
Ollal ameongeza kuwa changamoto nyingine ni kuchelewa kwa vifaa kulikosababishwa na upungufu wa fedha za kigeni katika manunuzi nje ya nchi.
Sambamba na Mhe.Waziri kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Mhandisi Yahya Samamba , Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo pamoja na maafisa mbalimbali kutoka wizara ya madini.
0 Comments