Na mwandishi wetu
Kizimkazi. Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS limeendelea kuwa kivutio baada ya kuongezwa zao jipya la utalii tofauti na ilivyokuwa katika matamasha ya miaka ya nyuma ya Kizimkazi.
Zao hilo jipya la Utalii wa Nyuki (Api-tourism) linalohusisha kudungwa na nyuki, na mazao ya nyuki yaliyoongezewa thamani kama vile asali, chavua, karanga za asali, maziwa ya nyuki ambavyo watu hutumia kama dawa na virutubisho katika mwili limeonekana kuwa kivutio sambamba na wanyamapori hai kama vile simba, chui, fisi, pundamilia na pofu.
Zao jipya la Utalii wa Nyuki (Api-tourism), linalojumuisha shughuli za kudungwa na nyuki na mazao ya nyuki yaliyoongezewa thamani kama vile asali, chavua, karanga za asali, na maziwa ya nyuki ambavyo hutumika kama dawa na virutubisho vya mwili vimekuwa kivutio kikubwa sambamba na wanyamapori hai kama vile simba, chui, fisi, pundamilia, na pofu.
Akiongea mara baada ya kuwapokea viongozi na wageni mashuhuri bandani hapo jana Agosti 20, 2024, Ephraim Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) amesema ikiwa ni siku moja kabla ya kuazimisha Siku ya Utalii katika Tamasha la Kizimkazi ameshuhudia umati mkubwa ukifika kudungwa na nyuki tofauti na zamani.
“Mapema mwaka huu Tanzania na China zilitiliana saini Itifaki ya kuuza Asali ya Tanzania nchini China na kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa ya kuzalisha asali yenye ubora kwa wingi ili kuinua vipato vyao na uchumi wa taifa kwa ujumla.
“Lakini mbali na hayo tumewaleta wananchi zao jipya la utalii wa nyuki, tumekuja na mzinga uliojaa nyuki, tunawadungisha watu, na mimi mwenyewe leo nimedungwa mara mbili, sijavimba na wala mkono hauniumi, na kama unavyoona mwitikio ni mzuri wananchi wanachangamkia fursa ya kudungwa, tena huduma hii tunaitoa bure jambo ambalo huwezi kupata sehemu nyingine,” anasema.
Brenda Mwakipesile ni moja kati ya wahifadhi wanaodungisha nyuki mamia ya wananchi wanaoendelea kumiminika kutembelea banda kuu la Wizara ya Maliasili na Utalii anasema kuwa, utalii huo mpya nchini umekuwa kivutio kwa wananchi wengi kutokana na kuwa ni tiba ya asili inayosaidia kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya maradhi mbalimbali na ustawi wa afya kwa ujumla.
Miongoni mwa wananchi waliojitokeza ni mhamasishaji maarufu na machachari wa mitandaoni Dotto Keto, maarufu kama Dotto Magari ambaye mara baada ya kudungwa na nyuki aliwaasa wananchi kuja kujionea maajabu ya utalii huo mpya wa nyuki, ili kupata fursa ya kujidunga bure na nyuki ndani ya viwanja vya Kizimkazi, akisema kuwa hii ni nafasi adimu na yenye faida nyingi kwa afya.
“Jamanii njoo Kizimkazi muone utalii wa nyuki, ma’nake nyuki tunawaogopa lakini hapa kuna binti jasiri, anawashika anawatuliza, nimedungwa safi kabisa, huu utalii wetu kiboko! Mkurugenzi Mafuru upewe maua yako,” anasema.
Tamasha la Kizimkazi lilianza mwaka 2015 ikiwa ni sherehe ya kumuaga Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais John Magufuli na baada ya kuteuliwa alikutana na wananchi wa Kizimkazi na kufanya sherehe ya kumuaga mwaka 2016 iliyojulikana kwa jina la Samia Day na ilipofika nwaka 2017 jina likabadilishwa na kuwa Kizimkazi day.
0 Comments