WITO WATOLEWA WAKULIMA KUCHANGAMKIA FURSA ZINAZOTOLEWA KUPITIA WIZARA YA KILIMO

 


Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni ya Kilimo ni Mbolea katika Mkoa huo tarehe 28 Agosti, 2024





Elimu ya Matumizi sahihi ya mbolea na usajili wa wakulima vyawavutia wakulima Katavi 


Wakulima nchini wametakiwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.


Aidha, wakulima wametakiwa kuacha kilimo cha mazoea na kufuata kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kutumia mbolea kwa usahihi.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela aliyezungumza  kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mwanamvua Mrindoko aliyekuwa kwenye majukumu mengine wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Kilimo ni Mbolea mkoani humo tarehe 28 Agosti, 2024.

"Niwasihi wakulima wote nchini wakiwemo wa mkoa huu wa Katavi kuchangamkia fursa zinazotolewa kupitia sekta ya kilimo ili muweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ya Jemedari Dkt. Samia Suluhu Hassan" Msovela ameongeza.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Eliurd Mwaiteleke amesema, matumizi ya mbolea kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni zaidi ya asilimia 75 ya mbolea zote zinazoingizwa nchini na kuzalishwa na viwanda vya ndani.

Amesema, mikoa inayoongoza kwa matumizi ya mbolea katika kanda hiyo ni pamoja na Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Rukwa na Katavi.

Ameongeza kuwa, kwa msimu wa kilimo 2023/2024 jumla ya wakulima 14,677 kati ya wakulima 69,073 waliosajiliwa katika mfumo wa ruzuku ikiwa ni sawa na asilimia 21.2 walinunua mbolea za ruzuku kiasi cha tani 4,097.75 zenye thamani ya ya ruzuku kiasi cha shilingi bilioni 4.5.

Amesisitiza kuwa, Serikali imekuwa ikisisitiza matumizi sahihi ya mbolea ili kuwafanya wakulima walime eneo dogo na kuvuna mazao mengi kwani ongezeko la watu duniani linapunguza eneo ambalo lingeweza kutumika kwa shughuli za kilimo.

Mwaiteleke alimalizia kwa kuuomba uongozi wa Mkoa wa Katavi na wadau wa kilimo kuunga mkono kampeni ya Kilimo ni Mbolea ili kuwaeleimisha wakulima na kuwahamasisha kuondokana na kilimo cha mazoea kisichokuwa na tija ili waweze kujikwamua kiuchumi.


Kwa upande wake mkulima wa mahindi, Frenk kibigas ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuweka nguvu kwenye sekta ya kilimo kwa kutoa ruzuku ya mbolea na kuwezesha upatikanaji wa vipimia udongo ili kuwafanya wakulima kutumia mbolea sahihi kulingana na mahitaji ya udongo na hivyo kuongeza uzalishaji


Chiku Mlisho ni mkulima wa mahindi  mwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 4 katika kijiji cha Igalula, Mpanda Ndogo, wilayani Tanganyika ameeleza kufurahishwa na  huduma ya kuhuisha taarifa zake zitakazo muwezesha kupata mbolea ya ruzuku msimu ujao baada ya kuongeza ekari ukubwa wa shamba kutoka ekari 4 hadi 6 na hivyo kukuza uchumi wake.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela (kushoto) akipewa maelezo ya namna wanavyosajili wakulima  na Afisa ugani Neema Mbuya (wa pili kulia) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuelimisha umma juu ya matumizi sahihi ya mbolea na kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ifukutwa, Kijiji cha Ifukutwa, Katavi ndogo mkoani Katavi tarehe 28 Agosti, 2024


Afisa Ugani Hamisi Seif (kushoto) akimwandikisha kwenye daftari la wakulima Amisa Hassan Said (kulia) aliyefika katika viwanja vya shule ya msingi ya Ifukutwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi tarehe 28 Agosti, 2024


Post a Comment

0 Comments