WMA YAELEZA FURSA ZA UWEKEZAJI KWA SEKTA BINAFSI

 


*Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo, Alban Kihulla (kulia) akimpatia maelezo ya majukumu ya Kituo cha Uhakiki wa Vipimo kilichopo Misugusugu, Mkoa wa Pwani, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Raphael Maganga, alipotembelea Kituo hicho Agosti 15, 2024.*


 *Veronica Simba na Paulus Oluochi – WMA* 


Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla ametaja fursa kadhaa za uwekezaji unaoweza kufanywa na sekta binafsi katika tasnia ya vipimo nchini Tanzania.


Kihulla ameeleza fursa hizo kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga aliyetembelea Kituo cha Uhakiki wa Vipimo kilichopo Misugusugu, Mkoa wa Pwani, Agosti 15, 2024.


Miongoni mwa fursa alizozitaja ni pamoja na sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa mizani mbalimbali na mita za maji, vifaa ambavyo amesema kwa sasa havizalishwi hapa nchini bali huagizwa kutoka nje ya nchi.


Amesema kuwa, Sheria ya Vipimo, Sura Namba 340 imeainisha fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta hiyo na kuongeza kwamba anaamini kupitia sekta binafsi, mita za maji na mizani mbalimbali zinaweza kuzalishwa hapa nchini na Wakala wa Vipimo ukabaki na jukumu lake la uhakiki wa vipimo hivyo.


“Sisi jukumu letu linakuwa zaidi kwenye uhakiki wa vipimo. Kwa sasa bado maeneo mengi yanahitaji vipimo vitumike, mathalani kwenye kilimo, mizani zinahitajika kwa wingi hivyo ni fursa kwa wenzetu wa sekta binafsi,” amesema Kihulla.


Aidha, ameongeza kuwa, sekta binafsi ikifanyia kazi fursa za uwekezaji alizoziainisha, itasaidia kutengeneza ajira kwa vijana ambao wanahitimu kutoka vyuo mbalimbali. “Utaalamu wao unaweza kutusaidia sisi kama Serikali kupitia Wakala wa Vipimo,” amefafanua.


Akieleza zaidi kuhusu majukumu ya WMA, Kihulla amesema utekelezaji wake ni sehemu ya kusimamia Ilani ya Chama Tawala inayoitaka Wakala hiyo kuhakiki kwa ufanisi vipimo vyote vinavyotumika nchini ili kuzilinda pande zote mbili zinazohusika yaani walaji na wafanyabiashara au wakulima.


Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TPSF ameipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa kituo hicho cha uhakiki wa vipimo ambacho kinatajwa kuwa cha aina yake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.


“Tunaipongeza Serikali kwa hatua hii kubwa lakini pia tunawahamasisha wafanyabiashara wanaotumia bidhaa kama mita za umeme, dira za maji, mizani mbalimbali na matanki ya kuhifadhi vimiminika jamii ya petroli kuvihakiki kupitia wataalamu wetu wa WMA ili wao wasipunjwe na pia wasiwapunje wateja wao.”


Akizungumzia lengo la ziara yake katika Kituo hicho, Maganga amesema ni kufuatia kikao cha wafanyabiashara wanaojishughulisha na vipimo kilichoketi yapata wiki mbili hadi tatu zilizopita ambapo kupitia majadiliano, walitamani kujua ni kwa namna gani huduma hizo zinaweza kuwafikia wengi zaidi na kwa njia rahisi zaidi.


Kituo cha uhakiki wa vipimo Misugusugu kinamilikiwa na Serikali kupitia Wakala wa Vipimo ambapo kinajihusisha na uhakiki wa dira za maji, mita za umeme na matanki ya malori yanayobeba vimiminika jamii ya petroli.


Kituo hiki hufanya kazi saa 24 kwa siku na kina uwezo wa kuhakiki malori 60 ya vimimika jamii ya petroli na dira za maji 800 kwa siku moja kwa kutumia teknolojia za kisasa, hivyo kukifanya kuwa cha kipekee Afrika ambapo hivi karibuni kumeshuhudiwa wageni kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanaokitembelea kwa ajili ya kujifunza.


*Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) Alban Kihulla (kulia) akimwongoza Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Raphael Maganga (kushoto), kutembelea Kituo cha Uhakiki wa Vipimo kilichopo Misugusugu, Mkoa wa Pwani, Agosti 15, 2024. Katikati ni Meneja wa Kituo hicho, Charles Mavunde.*


*Mtaalamu wa Wakala wa Vipimo (WMA), akihakiki gari la kubebea vimiminika jamii ya petroli katika Kituo cha kuhakiki vipimo kilichopo Misugusugu, mkoani Pwani. Taswira hii ilichukuliwa wakati wa ziara ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Raphael Maganga, Agosti 15, 2024.*



*Majengo yenye vifaa vya kitaalamu kwa ajili ya uhakiki wa vipimo mbalimbali yaliyopo katika kituo cha uhakiki wa vipimo Misugusugu, Mkoa wa Pwani, kinachomilikiwa na Serikali kupitia Wakala wa Vipimo (WMA). Taswira hizi zilichukuliwa wakati wa ziara ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Raphael Maganga, Agosti 15, 2024.*


Post a Comment

0 Comments