BASHUNGWA AONGOZA HARAMBEE UJENZI WA UKUMBI NA VYUMBA VYA KULALA WAGENI PAROKIA YA KASUMO; ZAIDI YA MIL 45 ZAKUSANYWA

 






Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (Mb) ameshiriki Misa Takatifu na kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa ukumbi na vyumba vya kulala wageni katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani Jimbo Katoliki la Kigoma ambapo zaidi ya shilingi Milioni 45 zimekusanywa.


Harambee hiyo imefanyika Mkoani Kigoma tarehe 20 Septemba, 2024 ambapo pamoja na mambo mengine, Waziri Bashungwa amemshukuru  Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma Mhashamu Joseph Mlola kwa kumpa fursa hiyo ya pekee kushiriki Ibada ya Misa na kuongoza Harambee katika Kanisa la Kasumo ambalo umisionari wake ulianza mwaka wa 1985.


Waziri Bashungwa amelipongeza Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma kwa uwekezaji wanaoendelea kuufanya pamoja na  kutoa elimu bora kwa vijana katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Rufino na Ronaldo na kuifanya shule hiyo kuwa na ufaulu mzuri.


Viongozi Wakuu waliochangia katika Harambee hiyo ni pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Doto Biteko, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Maji Eng. Kundo Mathew, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Eng. Maryprica Mahundi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye pamoja na viongozi wengine wa Serikali.


Bashungwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuufungua Mkoa wa Kigoma na Mikoa ya Kagera, Tabora na Katavi kwa barabara za lami ambapo katika miradi inayotekelezwa mkoani humo Wakandarasi wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana.


Akisoma Risala kwa niaba ya waumini wa Parokia ya Kasumo, Katibu wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo Bw. Onesmo Witae ameeleza kuwa hadi sasa wameweza kukusanya zaidi ya Shilingi Milioni 62 kutoka kwa wadau na marafiki wa Parokia hiyo kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi na vyumba vya kulala wageni katika Parokia hiyo.









Post a Comment

0 Comments