Na mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya Mbinga Mhe. Kisare Makori leo tarehe 6-9-2024 ametembelea eneo la ujenzi wa mradi wa shule ya sekondari mpya ya kisasa ya kata ya Litembo. Lengo la ziara hiyo ni kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa shule mpya katika kata hiyo.
Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 560 ambazo zimetolewa na serikali kuu ikiwa ni muendelezo wa mpango wa serikali ya awamu ya sita kuhakikisha kata zote za wilaya ya Mbinga zinakuwa na shule za sekondari.
Mradi huo kwa sasa upo katika hatua ya msingi ya utekelezaji wake.
Akizungumuza na baadhi ya wananchi wa kata ya Litembo waliojitokeza katika eneo la mradi huo kwa ajili ya kujitolea kuchimba msingi , Mkuu wa Wilaya amemushukuru sana Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia wilaya ya Mbinga jumla ya shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya za sekondari katika kata ya Litembo na Nyoni.
Aliendelea kusema kwamba ni ukweli usiopingika kwamba tunaye Rais ambaye amejitolea kidete katika kuhakikisha anasogeza na kufikisha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wake kama ambavyo alihaidi na sisi Mbinga ni mashahidi tumeletewa sh milioni 560 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya kisasa ya Litembo na shilingi milioni 560 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Nyoni.
Aidha Mkuu wa Wilaya amewapongeza viongozi na wananchi wa kata ya Litembo kwa kushiriki kikamilifu na kujitokeza kuchangia nguvu zao katika utekelezaji wa mradi huo.
Mkuu wa Wilaya pia ametoa rai kwa viongozi wote wanaosimamia mradi huo kuhakikisha kwamba mradi unakamilika kwa wakati kama ambavyo imekwishaelekezwa na serikali na kuzingatia ubora na viwango katika utekelezaji wake.
0 Comments