RAIS DKT SAMIA ZIARANI KIKAZI CHINA

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 6 Septemba 2024 jijini Beijing, China.Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anashiriki mkutano huu kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China.

Jukwaa la FOCAC lilianzishwa mwaka 2000 na Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika. Tangu kuanzishwa kwake jumla ya mikutano ya Kilele (Wakuu wa Nchi na Serikali) nane (8) imefanyika. 

 Ambapo Serikali ya China imemteua Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhutubia kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC itakayofanyika tarehe 5 Septemba 2024, akiiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati akitoa taarifa hiyo kwa Waandishi wa Habari ambapo amesema Mikutano hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kubalishana kati ya China na nchi moja ya Afrika ambapo Mkutano huu wa 9 wa FOCAC utafungulia na Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China ambapo, hotuba yake ya ufunguzi itatoa uelekeo wa China katika uhusiano wake na nchi za Afrika.

Ameongeza kuwa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo utaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ataungana na Wakuu wa Nchi na Serikali wenzake kutoka Nchi zaidi ya 40 kati ya 54 za Bara la Afrika kushiriki Mkutano huo. 

Aidha, Mhe. Antonia Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Moussa Faki, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika watashiriki Mkutano huo.

Mkutano huo wa Kilele wa FOCAC utaongozwa na kauli mbiu isemayo “Kushirikiana ili Kuendeleza Usasa na Kujenga Jamii Bora ya China na Afrika kwa Mustakabali wa Pamoja” (Joining Hands to Advance Modernization and Build a High-Level China-Africa Community with a Shared Future). Kauli mbiu hii inalenga kuwahamasisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na China kujadili kuhusu masuala muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na China ili kuongeza kasi ya maendeleo kwa pande zote mbili.

Post a Comment

0 Comments