RAIS MWINYI:BIMA KWA WATALII INALENGA KUIMARISHA SEKTA YA UTALII ZANZIBAR

 



Na mwandishi wetu


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema hatua ya kuanzisha bima ya afya kwa watalii inalenga kuimarisha sekta ya utalii pamoja na kuandaa mazingira salama na rafiki kwa wageni wanaokuja nchini.

Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 26 Septemba 2024 Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Balozi mpya wa Italia nchini,  Mhe.Giuseppe Sean Coppola aliyefika kujitambulisha.

Aidha Rais Dk. Mwinyi amesema bima ya afya kwa watalii sio jambo geni kwani mataifa mengi duniani tayari wamekuwa na huduma hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inamjengea mtalii uhakika wa kupata huduma bora za afya, ulinzi wa ustawi wake ikiwemo kumuondoshea usumbufu anapopata tatizo lolote ikiwemo kupoteza mizigo yake au hati za kusafiria.

Amefafanua kwamba Serikali imekua ikibeba mzigo mkubwa wa gharama kwa wageni wanaoingia nchini hasa wanapougua, ajali wakati wengine vifo, hivyo ameeleza kuanzishwa kwa bima hiyo kutaipa Serikali unafuu.

Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi ameielezea Italia kuwa mdau mkubwa kwa maendeleo ya utalii wa Zanzibar kwani imekua ikipokea idadi kubwa ya wageni kutoka nchi hiyo, hivyo amezialika kampuni za uwekezaji kutoka Italia kuja kuwekeza Zanzibar kwenye sekta nyengine.

Kwa upande mwingine, Balozi Sean Coppola amemuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kushirikiana zaidi katika maeneo ya afya, utalii, usimamizi wa taka kwa kuzichakata na kuwa rasilimali zenye tija pamoja na maendeleo ya Uchumi wa Buluu ambao kwa Zanzibar umekua ni miongoni mwa sera kuu ya Uchumi.










Post a Comment

0 Comments