Watumishi Tume ya Madini Wafundwa

 



*Watumishi Tume ya Madini Wafundwa*

Watakiwa kuendelea kupendana na kuepuka makundi

Ubunifu, nidhamu ya kazi iwe nguzo kuu kufikia lengo


WATUMISHI wa Tume ya Madini wametakiwa kufanya kazi kwa umoja, weledi  na kuheshimiana ili kufikia lengo la makusanyo ya maduhuli la kukusanya shilingi Trilioni Moja katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.

Hayo yamesemwa leo  Septemba 24, 2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba katika kikao maalum na watumishi hao jijini Dodoma chenye lengo la kuweka mikakati ya kuboresha Sekta ya Madini.

Akielezea hali ya makusanyo ya maduhuli tangu kuanza kwa mwaka mpya wa fedha, amesema kuwa katika kipindi cha mwezi wa saba na wa nane fedha iliyokusanywa haijawahi kukusanywa tangu  kuanzishwa kwa Wizara ya Madini na kuongeza kuwa matarajio ya mwezi huu wa tisa mambo yatakuwa mazuri  zaidi.

“Tunapaswa kukusanya  shilingi Bilioni 84 kila mwezi,  kwa miezi miwili tumekusanya wastani wa shilingi Bilioni 163.8, bei  ya dhahabu kwenye soko la dunia imepanda, lakini haina maana kama  hakuna udhibiti wa utoroshaji wa  dhahabu,”amesema Mhandisi Samamba.

Amesema kiasi hicho cha fedha cha shilingi Bilioni 163.8 kimepatikana  kutokana na udhibiti wa mianya ya upotevu wa makusanyo na kuimarisha usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.

“ Kila mmoja atekeleze wajibu wake, tukiweza kufanya hivi tutafika lengo la kukusanya  shilingi Trilioni Moja na lengo hili litafikiwa kama wote  tukiendeleza umoja na upendo hasa ikizingatiwa muda mwingi tunakuwepo pamoja ofisini,” amesisitiza Mhandisi Samamba

Ameongeza kuwa Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini itaendelea kuboresha mazingira ya kazi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha na vifaa vya kutosha kama mkakati wa kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unaendelea kukua.














Post a Comment

0 Comments