BASHUNGWA ATAKA WANANCHI WARUHUSIWE KUTUMIA BARABARA ZA BRT AMBAZO HAZINA MABASI.

 



Na mwandishi wetu

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kukutana na Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Jeshi la Polisi pamoja na Wakala ya Barabara (TANROADS) kuratibu namna ya kuwawezesha Wananchi kutumia miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) iliyokamilika kujengwa na haijaanza kutumiwa na Mabasi ya Mwendokasi ili kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam hususan majira ya asubuhi na jioni.

Bashungwa ametoa kauli hiyo Oktoba 22, 2024 Mkoani Dar es Salaam wakati akieleza maendeleo ya Ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka na kueleza kuwa ipo miundombinu ya BRT iliyokamilika lakini imefungwa ili kusubilia Mabasi yaletwe ambapo ametaka uweke utaratibu wa kuwawezesha Wananchi kutumia barabra hizo wakati Mabasi ya Mwendokasi yakisubiliwa .

“Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam naomba hili nikuachie uratibu, haileti maana unakuta wananchi wapo kwenye foleni halafu katikati barabara ni nyeupe haitumiki, naona haja ya kuweka utaratibu ambao utasaidia kupunguza foleni kwa kipindi hiki majira ya asubuhi na jioni”, amefafanua Bashungwa.

Bashungwa amebainisha kuwa utaratibu huo ufanyike katika barabaara za Mwendokasi ambazo hazijaanzisha huduma yaa Mabasi ya Mwendokasi na pindi Mabasi  yakiletwa utaratubu urejee kama kawaida kwa kila Magari kupita katika barabara zake.

Aidha, Bashungwa ameeleza Serikali ipo hatua za manunuzi ya kumpata Makandarasi wa kuanza Ujenzi wa miundombinu ya BRT awamu ya tano ambao unahusisha barabara za Nelson Mandela, Kigogo, Tabata hadi Segerea na barabara ya Temeke.

Kadhalika, Ameeleza kazi ya Upanuzi wa barabara ya Morogoro kutoka Ubungo hadi Kimara inaendelea ambapo utekelezaji upo asilimia 16.






Post a Comment

0 Comments