BASHUNGWA AWEKA JIWE LA MSINGI SHULE YA SEKONDARI MSANGANI, AMPONGEZA RAIS SAMIA.

 




Na mwandishi wetu


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekagua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari   ya Msangani Government katika kata ya Msangani iliyopo Halmashauri ya Mji wa kibaha Mkoani Pwani ambapo Serikali imetoa kiasi cha shilingi Milioni 528.9 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Waziri Bashungwa akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ameweka jiwe la msingi leo tarehe 08 Oktoba 2024 na kuridhishwa na usimamizi na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa Shule hiyo ulioanza mwezi Juni, 2024.

Waziri Bashungwa amemshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu ya msingi na sekondari nchini ambapo katika kipindi cha miaka minne zimejengwa Shule za Msingi 10 na Shule za Sekondari 10 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

Bashungwa ameutaka Uongozi wa Shule na Kamati ya Ujenzi kuendelea kuusimamia kikamilifu ujenzi wa shule hiyo ili uweze kukamilika ifakapo mwezi Novemba, 2024 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kupokea wanafunzi mwezi Januari, 2025.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Msangani kutasaidia wanafunzi kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu na kuwa na mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia.

“Katika kata ya Msangani hii ni Sekondari ya pili kujengwa, wanafunzi wa maeneo ya Mugina walikuwa wanatembea umbali mrefu hivyo kukamilika kwa Sekondari hii, watatembea umbali mfupi na kupata elimu bora”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha kupima eneo la shule na kuwa na hatimiliki pamoja na kuratibu wananchi kujenga kwa kuzingatia mipango miji itakayopendezesha mji wa Kibaha na kuepuka ujenzi holela.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema Mheshimiwa Rais Dkt. samia Suluhu Hassan ameshapeleka kiasi cha shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Sekta zote katika Mkoa wa Pwani.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon ameeleza kuwa Wilaya ya Kibaha inapokea takribani Bilioni 11 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo zinawezesha ujenzi wa Shule tatu kila mwaka ambapo wamepanga kujenga Shule katika Kata za Pangani, Tangiri na Msangani.

Akitoa taarifa ya mradi, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Msangani Government, Lilian Marandu ameeleza kuwa ujenzi wa miundombinu katika Shule mpya ya Sekondari ya Msangani unaendelea na upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na hadi sasa kiasi cha Shilingi Milioni 175.704 zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali.








Post a Comment

0 Comments