GEITA YATIKISA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

 




Na mwandishi wetu

● Wananchi wamshukuru Rais , Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi


●Miradi ya maendeleo yatekelezwa kwa asilimia 90


⚫️ Wilaya ya Mbogwe na Bukombe zapiga hatua kubwa kimaendeleo


●Sekta ya Madini Geita ya kinara katika kuchangia fedha.


*MBOGWE  & BUKOMBE - GEITA*

Wananchi katika  Wilaya za Mbogwe na Bukombe mkoani Geita wameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi na kuchochea upatikanaji wa maendeleo kwa kasi.

Hayo yamebainika jana Oktoba 8, 2024 katika muendelezo wa  ziara ya kukagua na kuzindua miradi ya  maendeleo wilayani Mbogwe na Bukombe inayofanywa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde mkoani Geita kwa niaba ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan.

Dkt.Zakayo Sungura akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa hospitali Wilaya ya Mbogwe, amesema kuwa , kuanzia mwaka wa 2019/2020 mpaka kufikia mwaka wa 2024/2025 zaidi ya bilioni 2.7 zimepelekwa kwa ajili utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa hospitali katika  kata ya Mbogwe.

Dkt.Sungura ameishukuru serikali kwa kukamilisha ujenzi wa hospitali  ya wilaya pamoja kupokea vifaa tiba vitakavyo saidi wananchi wa Mbogwe na maeneo ya karibu kwa kuwa awali iliwalazimu kwenda Wilaya ya kahama kupata huduma hizo.

Akitoa taarifa  ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mkuu wa  Wilaya ya Bukombe Mhandisi  Paskasi Muragili amesema kuwa kwa kipindi cha miaka 3 Wilaya ya Bukombe imepokea fedha za miradi ya maendeleo takribani Tsh 45 bilioni ambazo zimewekezwa kwenye sekta ya  Afya, Barabara ,  Nishati ya umeme na sekta ya elimu.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mh. Martin Shigella amemshukuru Mh. Rais Samia kwa utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo kufikia zaidi ya Tsh 800 bilioni kwa kipindi cha miaka mitatu na kusema kwamba miradi hiyo imesaidia kuchochea ukuaji wa kasi wa Mkoa wa Geita.

Akizungumza na Wananchi wa Wilaya za Bukombe na Mbogwe Waziri Mavunde amesema  kuwa Mkoa wa Geita ni kati ya mikoa iliyopokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwenye nyanja ya Afya,Elimu,Miundombinu,Nishati na uwezeshwaji wananchi kiuchumi.

“Mh. Rais Samia amefanya kazi kubwa sana mkoani hapa,nimeona idadi ya shule mpya nyingi zimejengwa,nimeziona Hospitali za Wilaya,Vituo vya Afya na Zahanati kila kona,nimeona barabara mpya za lami,miradi ya maji na utekelezaji wa kupeleka umeme vijijini.

Ni dhahiri kwamba wanaGeita mtakubaliana na mimi kiasi cha Tsh 800 bilioni kilicholetwa mkoani hapa tunauona utekelezaji wa kweli wa miradi ya maendeleo”Alisema Mavunde

 Waziri Mavunde pia aliupongeza mkoa wa Geita kwa kuwa kinara katika kuchangia kwenye sekta ya madini ambapo kwa mwaka wa 2024/2025 imepanga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 246.

Waziri Mavunde yupo mkoani Geita kwa ziara ya kikazi ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo mkoani Geita.


Post a Comment

0 Comments