MASHINE YA XRF NDIO MPANGO MZINA KATIKA MAONESHO YA MADINI GEITA

 



_Katika Maonesho ya Madini Geita…_

*Mashine ya XRF ndio mpango mzima*

_Viongozi na  wananchi wamiminika kupima madini yao_

*Geita*

Wadau wa madini wahamasishwa kutumia Maabara ya Tume ya Madini 

VIONGOZI na wananchi mbali mbali wameendelea kujitokeza  kupata elimu kuhusu madini yaliyopo katika miamba na namna ya kupima sampuli za madini ya metali   kwenye  mashine ya XRF katika Banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Saba ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea kwenye viwanja vya Bombambili mkoani Geita.

Mashine hiyo ni maalum kwa kupima madini ya metali kwa njia ya mionzi /X-RAY na kisha kukupa majibu kwa kukuonyesha kiwango cha madini yote yaliyomo ndani ya metali hiyo kwa asilimia.

Akitoa elimu hiyo kwa viongozi na wananchi Afisa Maabara kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Edith Lewis amesema kuwa madini yapo ya aina nyingi  duniani lakini  huwa hayakai yenyewe, lazima yanakuwa yamechanganyikana na aina mbalimbali nyingine za madini katika miamba

Amesema,  watu  wanaonunua dhahabu ambao wanaogopa kutapeliwa kwa kuuziwa dhahabu feki wafike kwenye banda la Tume ya Madini kupata elimu ya namna ya kutambua miamba na madini mbalimbali  pia wanaweza kupima hereni, mikufu ya dhahabu na shaba katika banda na  kushauri wananchi kuitumia fursa hii kufika katika maabara ya Tume madini iliyopo Msasani- Tirdo Complex jijini Dar es Salaam ili kupima sampuli zao.

“Hii mashine ina kioo maalum itakuonyesha kwenye kioo madini yaliyomo ndani mfano ukipima dhahabu baada ya mionzi kuscan itakuonyesha dhahabu ipo asilimia 11 na Shaba ipo asilimia 89 sasa wewe  ukiona hivi  unajua moja kwa moja ulichouziwa ni feki ama si feki.

Amesema pia kuna mashine ya kupima sampuli za miamba kwa njia ya mionzi ambayo inatoa majibu ya ‘elements’ zote zilizomo kwenye huo mwamba na majina yake na wingi wake kwa kukuwekea asilimia yaani kama ni shaba  utaona itaandika "Cu....%, kama ni madini ya chuma itaandika "Fe"....% kama ni dhahabu ipo itaandika "Au"....%.

Aidha, Mhandisi Edith ametoa wito kwa wananchi  wanaofika  kwenye maonesho ya Madini Geita  kutembelea banda la Tume ya Madini ili pia kujionea vito mbali mbali na kujifunza fursa zilizopo katika sekta ya madini.

Kauli mbiu  ya mwaka 2024 katika Maonesho ya Saba ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini  ni  Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Nishati Safi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Endelevu’.

Baadhi ya viongozi waliotembelea Banda la Tume ya Madini na kupata elimu ya upimaji sampuli ni  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, Mbunge wa Geita Mjini Constantine Kanyasu ambae pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Viongozi wengine waliotembelea banda la Tume  ni pamoja na  Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mkurugenzi wa Blue Coast Ignas Inyasi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse,  Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe, Dkt. Jacob Julius na  Mwenyekiti wa UVCCM Geita Manjale Magambo.
















Post a Comment

0 Comments