MBUNGE WA LUDEWA AIPA KONGOLE TARURA

 


Na mwandishi wetu


#Zaidi ya bilioni 13 zaboresha miundombinu vijijini


Ludewa,Njombe 

Bunge wa Ludewa (CCM) Mhe. Joseph Kamonga  ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)  kwa kutenga asilimia thelathini ya fedha kwaajili ya kuviwezesha vikundi kazi vya kijamii  ambavyo vinajishughulisha na matengenezo madogo madogo ya miundombinu wilayani hapo.

Pongezi hizo amezitoa mbele ya waandishi wa habari mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya Ujumbe Maalum  kutoka Jamhuri ya Sierra Leone uliofika  kujifunza namna vikundi vya kijamii vinavyofanya kazi za ujenzi na matengenezo madogo madogo ya miundombinu ya barabara katika Kata ya Lugarawa, Wilayani Ludewa.

Mhe. Kamonga alisema kwamba njia hiyo ni namna bora inayofanywa na Serikali kupitia taasisi zake  kwa kurudisha kipato kwa jamii na kwamba imeleta ajira kwa wananchi wa eneo husika na kuisaidia jamii kwani fedha hizo zinawafikia watu wengi.

“Ninayo furaha kubwa sana ya kuwapokea wageni hawa hapa Ludewa na wamejionea namna jamii inavyoshirikishwa katika miradi ya Serikali kwenye ujenzi wa makaravati na matengenezo madogo madogo ya barabara”.

“Tarura wamewapa mafunzo mbalimbali ya namna ya kufanya  matengenezo ya barabara, ujenzi wa makalavati pamoja na madaraja, njia hii ni nzuri kwa serikali kurudisha mapato kwa jamii kwani imeweza kuisaidia jamii kubwa kupitia kazi wanazofanya, tunawashukuru TARURA kwa kuichagua Ludewa”. Aliongeza Mhe. Kamonga.

Hata hivyo Mhe. Kamonga alisema kwamba TARURA katika jimbo lake wameweza kufungua barabara katika maeneo mengi ambayo tangu Uhuru hakukuwa na barabara akitolea mfano barabara ya mwenge hadi makonde hakukuwa na barabara kabisa ila hivi sasa wananchi wanayaona magari.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Olivanus Thomas alisema kwamba TARURA imeweza kutumia zaidi ya bilioni 13 kwaajili ya kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini kwa kujenga barabara za lami, changarawe na udongo  katika kipindi cha miaka mitatu chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wa ushirikishwaji wa jamii alisema wilaya yake kuna vikundi vipatavyo hamsini na mbili ambavyo vinawajumlisha wazee, vijana walemavu na wanawake ambavyo vimeweza kunufaika na fedha hizo zilizotengwa kwaajili ya vikundi kazi.

“Yapo mazuri mengi ambayo yanafanywa na Serikali nchi nzima kwani fedha za miradi zimepelekwa na kwa upande wetu Ludewa kwenye upande wa TARURA zimeweza kuwanufaisha wakandarasi wadogo na wakubwa kupitia pesa hizo”.

Aliongeza kusema kwamba kwa ujio  huo umekuwa na manufaa kwao kwani imekuwa ni historia kwa Tanzania hususan Ludewa wageni wamejionea na kujifunza mambo makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufikia malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.




Post a Comment

0 Comments