RAIS MWINYI: ZANZIBAR KUIMARISHA UHUSIANO NA WAKFU QATAR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akiwa anamaliza ziara yake ya siku mbili nchini Qatar leo Jumatano 30 Oktoba 2024 amekutana na Waziri wa Masuala ya Wakfu wa Qatar Mheshimiwa Shanem bin Shaheem bin Ghaneem Ghanim.
Rais Dk. Mwinyi aliishukuru Serikali ya Qatar kwa msaada mkubwa ilioutoa kufuatia janga la maporomoko ya udongo Wilayani Hanang Mkoani Manyara mwaka 2023.
Mfuko wa Wakfu unaosimamiwa na Waziri huyo ulisaidia kwa kiasi kikubwa waathirika wa janga hilo.
Aidha Rais Dk. Mwinyi amesema angefarajika zaidi kuona kunaimarishwa ushirikiano baina ya pande mbili za Wakfu upande wa Zanzibar na Qatar.
Dk. Mwinyi amemuomba waziri huyo kupitia mfuko wa Wakfu wa Qatar kuwasaidia wenzao wa Zanzibar kuwajengea uwezo hasa upande wa mafunzo ombo lililokubaliwa na Mheshimiwa Ghanem.
Rais Dk Mwinyi amemkaribisha Zanzibar Waziri huyo kujionea kazi za Wakfu zinavyofanyika.
Halikadhalika kuhusu Hijja Dk Mwinyi alimuomba Waziri huyo kusaidia Mahujaji wa Zanzibar ambapo Zanzibar hupatiwa nafasi za Kuhiji elfu kumi na mbili kwa mwaka lakini ni idadi ndogo tu ya mahujaji wanamudu kutekeleza nguzo hiyo muhimu ya Kiislamu.
Naye Waziri Ghanem amemuahidi Dk. Mwinyi kulifanikisha suala hilo kwani mwezi Januari mwakani atatembelea Saudia na na atazungumza nao namna ya kusaidia Mahujaji zaidi wa Zanzibar kushiriki Hijja
0 Comments