RAIS SAMIA KUTIKISA MIAKA 50 YA AICT.

 


Na mwandishi wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia mgeni rasmi maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Kanisa la AICT Pastoreti ya Magomeni   tangu lilipoanzishwa na kuanza kutoa huduma.

Akizungumza Waandishi wa habari leo Oktoba 17, 2024 Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Pwani Philipo Magwano Mafuja amesema

"Tarehe 27 Oktoba, 2024 Kanisa la AICT- Pastoreti ya Magomeni, ambalo ni Kanisa la Uaskofu tutakuwa na ibada ya Misa Maalum ya kumtukuza, kumsifu, kumuabudu na kumuomba Mungu tukiadhimisha Jubilee ya Miaka 50 (Golden Jubilee), tangu lilipoanzishwa na kuanza kutoa huduma," amesema Askofu Mafuja na kuongeza,

"Tunayo furaha kubwa kuwataarifu waumini wote wa AICT na Watanzania kwa ujumla kuwa, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekubali kujumuika nasi kwenye Misa hiyo, itakayoenda sambamba na harambee ya kukamilisha ujenzi wa Kanisa unaoendelea kanisani hapa, ambapo yeye ndiye mgeni rasmi,".

Hivyo Askofu Mafuja ametumia fursa hiyo kuwataarifu mamilioni ya waumini wa Kanisa hilo kote nchini na kuwaalika wajumuike katika ibada ya Misa Maalum ya kusherehekea Jubilee hiyo ya Miaka 50 ya Kanisa hilo.

"Shughuli hiyo itafanyika tarehe 27 Oktoba, 2024 ni tukio la furaha tunapoadhimisha Miaka 50 ya uaminifu wa Mungu Kwa kusanyiko la Kanisa la AICT Magomeni ambalo ni sehemu ya kusanyiko kubwa la waamini wa Kanisa la Africa Inland Church-Tanzania (AICT)," ameeleza Askofu Mafuja na kubainisha,

"Sisi Kanisa la AICT- Pastoreti ya Magomeni, tukiwa na washiriki wa mwili wa Kristo, tumepata Baraka nyingi na hatua muhimu katika safari Yetu hii ya Miaka 50. Pamoja na kufanya tafakuri, tumeona ni furaha na ibada njema kumrudishia Bwana shukrani, heshima, sifa na utukufu, Kwa ajili ya tulikotoka, tulipo na tuendako,".

Kwamba Misa hiyo Maalum itafanyika ndani ya Kanisa la AICT-Magomeni ambapo itaambatana na kumtukuza, kumsifu na kumwabudu Mungu Kwa mahubiri, nyimbo, maonesho Maalum, ujumbe Maalum Kutoka Kwa mgeni rasmi Rais Dkt. Samia na salamu za wasemaji wengine.

Ameongeza kuelekea siku hiyo Oktoba 27, 2024 watakuwa na shughuli nyingine za kiroho na kijamii kama vile kuwa na tamasha la uimbaji, maombi na shughuli za kijamii na matendo ya huruma na upendo Kwa Jamii ya Watanzania inayowazunguka.

Post a Comment

0 Comments