TANZANIA NA SINGAPORE KUIMARISHA UHUSIANO WAKE

 



Na mwandishi wetu

📌 *Zanuia Kuongeza Kiwango cha Ufanyaji  Biashara*


📌*Dkt. Biteko amwalika nchini Naibu Waziri Mkuu wa Singapore*


📌 *Singapore yasema iko tayari  kubadilishana uzoefu na Tanzania* 


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na Singapore  zitaenzi uhusiano uliopokati yake ambao umedumu kwa muda mrefu, kwa kuainisha sababu za uhusiano huo na kuongeza ufanyaji wa biashara kati ya nchi hizi mbili.

Dkt. Biteko ameyasema hayo Oktoba 21, 2024 akiwa nchini Singapore mara baada ya kukutana  na kufanya mazungunzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe. Gan Kim Yong.

“ Tunatakiwa kujifunza kutokana na uhusiano huu na hasa kutoka Singapore kwa kuwa mmepiga hatua katika sekta ya nishati hadi kuwa na uwezo wa kufikia mahitaji ya juu ya umeme ya zaidi ya Gigawati 8, hicho ni kiasi kikubwa ikilinganishwa na Tanzania yenye  takribani Megawati 3000 ambapo hadi mwaka 2030 tumepanga kufikia Megawati 10,000,” amesema Dkt. Biteko.

Amesisitiza “ Mpango huo hauwezi kutokea bila kuwa na ushirikiano na wadau na nchi zingine kama Singapore, ni matumaini yetu kuona ushirikiano huu unaendelea kukua kati ya nchi zetu na kuleta manufaa kwa wananchi”

Dkt. Biteko ameipongeza Singapore kwa uzalishaji wa umeme wa jua na kusema kuwa Tanzania inaendelea na jitihada zake za kuzalisha umeme huo.

Akitaja miradi ya nishati inayoendelea kutekelezwa, Dkt. Biteko amesema kuwa kwa sasa nchi inaendelea na utekelezaji wa mradi Julius Nyerere (JNHPP)utakaozalisha megawati 2115. 

Aidha, upembuzi yakinifu unaendelea kuhusu miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amemualika Naibu Waziri Mkuu wa Singapore, Mhe. Yong nchini Tanzania.

“ Kwa niaba ya Serikali na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tutafurahi ukija Tanzania na tuna amini kuna maeneo mengi ya kushirikiana nanyi,” amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Singapore, Mhe. Yong amesema kuwa nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuwa nchi hizo zina mahitaji ya kufanana.

Aidha, amesema kuwa Singapore inatumia zaidi gesi asilia kama chanzo cha nishati ingawa  pia inatumia umeme unaozalishwa kwa maji, jua na upepo. 

Vilevile amesema nchi yake  iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya nishati.

Post a Comment

0 Comments