DKT. KAZUNGU AKAGUA MRADI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME KUTOKA JNHPP HADI CHALINZE



Na mwandishi wetu

📌 *Apongeza kazi kubwa iliyofanyika katika kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme nchini.*


📌 *Mradi wafikia asilimia 97.38*


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu ametembelea mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze na kituo Cha kupoza umeme Cha Chalinze kwa ajili ya kukagua hatua ya utekelezaji wa mradi.

Akiwa katika eneo la mradi,  Chalinze mkoani Pwani, Dkt. Kazungu ametembelea maeneo yote ya mradi huo na kushuhudia kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO).

Dkt. Kazungu amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ambao  umegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka JNHPP hadi Chalinze yenye urefu wa kilomita 160 na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Cha Chalinze ambacho kinahusisha ufungaji wa transfoma sita zenye uwezo wa MVA 250 kila moja ni kiunganishi kikubwa katika kuhakikisha umeme unafika pande zote za nchi.

" Kakamilika kwa mradi huu kutasaidia umeme kutoka JNHPP kufika  pande zote zilizokusudiwa.TANESCO msimamieni Mkandarasi akamilishe kazi kwa ufanisi kwani umeme ni maisha na  uchumi ambao ukipatikana utafungua fursa za viwanda ambazo zitainua maisha ya mtu mmoja mmoja  na kukuza  uchumi nchini." Amesema Kazungu

Amesema malengo ya mradi huo ni pamoja na usafirishaji wa umeme ( 2,115 MW) utakaozalishwa katika Bwawa la JNHPP na kuufikisha Chalinze,vile vile lengo la pili ni kuwa na kituo Cha kupoza umeme Cha Chalinze kwa ajili ya kupokea umeme kutoka Bwawa la JNHPP na kuboresha upatikanaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa.

Ujenzi wa kituo Cha kupoza umeme cha Chalinze ulianza Mwezi Oktoba 2021 na utekelezaji wa mradi mpaka sasa umefikia asilimia 97.38, huku kazi za ufungaji wa mifumo ya kuendesha kituo zikikamilika na kwa sasa kituo kinapokea umeme unaozalishwa kutokea JNHPP na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.








Post a Comment

0 Comments