Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuongeza uwajibikaji na nidhamu ya kazi, kuboresha utendaji kazi na kuimarisha ushirikiano na viongozi ili kuendelea kudumisha amani, utulivu na usalama wa nchi.
Bashungwa ametoa wito huo, leo Januari 7, 2025 wakati akifungua mkutano wa Baraza Kuu la wafanyakazi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, jijini Dodoma, kililenga kushirikisha watumishi katika kupanga na kutekeleza malengo ya Wizara kwa pamoja.
Amewataka wajumbe wote kushiriki kikamilifu majadiliano na kutoa mawazo, ushauri na michango ambayo itasaidia uongozi wa Wizara kusimamia vema, na kwa ufanisi, utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Wizara.
“Michango yenu ilenge kutekeleza falsafa ya 4Rs za Mheshimiwa Rais, ambazo ni Maridhiano(Reconcialition), Mabadiliko (Reforms), Ustahimilivu (Resiliance) na Kujenga upya (Rebuilding)” Amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemshukuru Mhe. Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kuendelea kuiwezesha Wizara ya Mambo ya Ndani katika kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Kwa upande wake, Naibu wa Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo amewapongeza watumishi kwa kuendelea kuwa Wazalendo katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi mkubwa.
Nae, Mweyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu amasisitiza watumishi watumie baraza hilo kutoa michango yenye tija itakayowezesha Wizara kutekeleza majukumu ya kila siku.
"Kufanyika kwa Mkutano huu wa Baraza Kuu la wafanyakazi wa Wizara ni fursa kwa watumishi wote kushirikishwa katika kupanga mipango ya Wizara Kupitia majadiliano ya pamoja" Alisema Katibu Mkuu Gugu.
0 Comments