Na mwandishi wetu
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema Programu ya Kuwapatia Wanafunzi wa Kike Taulo za Kike ni Program Mama ya Taasisi hiyo na ni Endelevu.
Mama Mariam Mwinyi ambae ni Mwenyekiti wa Bodi na Msarifu wa Zanzibar Maisha Bora Foundation ameeleza kuwa taasisi hiyo itaendelea kuunga Mkono juhudi za Serikali za Kuwasomesha Wanafunzi wa Kike kwa ajili ya kutimiza ndoto zao kielimu.
Ameeleza kuwa Wanafunzi wa Kike Balehe wamekuwa wakikosa Masomo Siku 48 katika Mwaka Mmoja kutokana na Changamoto za Ada zao za Mwezi hali inayozorotesha juhudi zao na za Serikali za kuhakikisha Mwanafunzi wa Kike anakabiliana na changamoto za Skuli na kuweza kufikia ndoto zao.
Halikadhalika, Mama Mariam Mwinyi ameeleza kuwa tayari wamewafikia Wanafunzi 1,762 katika Kampeni yenye lengo la kuwafikia Wanafunzi 3000 Nchi nzima wakiwemo Wanafunzi 342 wa Skuli ya Sekondari ya Ole ambao amewakabidhi Taulo za kike ambazo zikitumika Vizuri zinaweza kutumika kwa Takriban Miaka Mitano.
Hatua hiyo imewezesha kufikia Wanafunzi wa kike 8,676 kuendelea na masomo bila kuyakatisha kwa utoro na kuwapunguzia Gharama Wazazi za ununuzi wa Taulo za kike.
Vilevile , Mama Mariam Mwinyi ameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuimarisha Mazingira ya usomaji katika skuli mbalimbali kwa kuwepo kwa huduma za Maji safi tiririka na salama , ujenzi wa vyoo na mazingira mazuri ya kusomea kwa Wanafunzi wa Kike kupitia Mradi wa SWASH pamoja na Taasisi ya Infinity Foundation kwa kuwa mstari wa mbele katika Kampeni hiyo endelevu.
0 Comments