MWANA FA: KAMA HAUJACHEZA 'AMATEUR' MARUFUKU KUCHEZA NGUMI ZA KULIPWA

 


Na mwandishi wetu

Naibu waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo mhe. Hamis Mwinjuma ametoa maagizo kwa mamlaka ya ngumi za kulipwa nchini Tanzania TPBRC ili kuongeza ufanisi katika mchezo huo.

Akiongea leo na waandaaji wa mapambano na viongozi wa TPBRC katika kikao kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam mhe. Mwinjuma amesema TBPRC wanatakiwa kutenga idadi maalumu ya mapambano wanayotakiwa mabondia kupigana kwenye ngazi ya ridhaa kabla ya kuingia kwenye ngumi za kulipwa.

Mhe. Mwinjuma amefuta vibali vinavyotolewa kwa mabondia wanavyopatiwa wakiwa uwanja wa ndege wakati wanapokwenda nje ya nchi kupigana na amewataka mabondia kufuata utaratibu rasmi uliowekwa.

Mhe. Mwinjuma amesema waandaaji wa mapambano kabla ya kuingia mikataba na mabondia wawe wamewapima mabondia hali zao za kiafya ili kuepuka matatizo ambayo yanawakuta mabondia kwenye mchezo wa ngumi.

Kuhusu suala la bima ya afya kwa mabondia mhe. Mwinjuma ameamua kulivalia njuga suala hilo kwa kuona namna ya kuzungumza na makampuni ya bima ili kuja na ufumbuzi.

"Nitazungumza na makampuni ya bima ili kuweza kuwakava mabondia kwaajili ya bima ya afya wakati wa maandalizi, wakiwa ulingoni na siku kadhaa baada ya pambano.

"Hili nitalifanya mimi na baraza la michezo watawafahamisha kamisheni mchakato utakavyokua lengo ni kuwa na mpango maalum wa kuwalinda mabondia kwenye suala la bima ya Afya," amesema mhe. Mwinjuma.

Na kwa upande wa maoni yaliyotolewa na wadau wa ngumi katika kikao hiko kuhusu kuingiza mchezo wa ngumi kwenye mashindano ya mashule ikiwemo UMISETA na UMITASHUMTA mhe. Mwinjuma amesema jambo hilo lina ukakasi kulingana na uhatari wa mchezo wenyewe kwa watoto.

"Suala la kuingiza mchezo wa ngumi kwenye UMISETA na UMITASHUMTA limekua na ukakasi kulingana na mchezo husika kwa watoto wadogo kupigana inaweza kuwa ni hatari. sijui natakiwa niseme maneno gani ili wenzetu wa Wizara ya elimu na TAMISEMI wanielewe kwamba nataka niweke ulingo watoto wapigane,"amesema naibu waziri huyo.

Credit @daukasomba29

Post a Comment

0 Comments