Mbunge Njombe Mjini Aitaka Serikali Kusimamia Vibali kwa Wawekezaji wa Misitu

 




Na Mwandishi Wetu, Dodoma

14 Aprili 2025


Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, Mhe. Deo Mwanyika, ameishauri serikali kutokuwa na haraka kutoa vibali kwa wawekezaji wa sekta ya misitu wasiowekeza katika kuongeza thamani ya mazao ya misitu mkoani Njombe.

Akichangia Hotuba ya Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma, Mhe. Mwanyika aliipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, ikiwemo sekta za elimu, afya, maji, barabara, na umeme vijijini.

Katika sekta ya maji, Mbunge huyo alibainisha kuwa miradi ya Ijunilo na Livingstone tayari imekamilika na inaendelea kutoa huduma ya maji kwa wakazi wa Mji wa Njombe, hali iliyosaidia kupunguza mgao wa maji. Aidha, miradi ya Hagafilo na ya majitaka inaendelea na itakapokamilika, inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi wa mji huo.

Kuhusu umeme, alisema vijiji vyote katika jimbo lake tayari vimeunganishwa na huduma hiyo, na kwa sasa juhudi zinaelekezwa katika vitongoji. Alitoa wito kwa serikali kuhakikisha maeneo ya Ihanga-Itulike, Mpumbwe-Maheve, Ukwelela-Wikichi na Unguja-Kambarage yanapatiwa huduma hiyo kwa haraka.

Mbunge huyo pia aliishukuru serikali kwa hatua ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, vituo vya afya, zahanati pamoja na kuanzishwa kwa tawi la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mkoani humo. Aidha, alieleza matumaini yake juu ya mchakato unaoendelea wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa mjini Njombe.

Katika hoja ya uwekezaji, Mhe. Mwanyika alitaka serikali kuwa makini na mikataba inayosainiwa na wawekezaji, akitolea mfano wa mwekezaji wa chai ambaye alidai kuwa amekuwa kikwazo kwa wakulima kutokana na kushindwa kuwalipa kwa wakati, hali iliyopelekea baadhi ya viwanda kusimama kazi.

“Tunashuhudia pia wawekezaji wengi wa mazao ya misitu wakinunua mazao kwa bei ya chini sana, bila mpango madhubuti wa kuhamasisha upandaji wa miti. Hii inamnyima mkulima wa miti tija stahiki,” alisema. Alipendekeza vibali vya uchakataji wa mazao ya misitu visitolewe kwa wawekezaji ambao hawajaonyesha nia ya kuwekeza kwenye uongezaji thamani, akitoa mfano wa kampuni ya TANWATT inayofanya kazi kwa tija mkoani humo.

Mwisho, alielezea matumaini yake kwa serikali kuhusu mradi wa Liganga na Mchuchuma, akisema hatua ya mazungumzo inayoendelea na mwekezaji ni hatua nzuri kuelekea kuinua uchumi wa mkoa wa Njombe na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments