Mwambisi Forest Yashinda Milioni 50 Kampeni ya Upandaji Miti ya NMB

 






Na Mwandishi Wetu, Kibaha


Shule ya Sekondari ya Mwambisi Forest iliyopo Kibaha, mkoani Pwani, imeibuka mshindi wa kwanza kitaifa katika kampeni ya upandaji miti iliyoandaliwa na Benki ya NMB, na kuzawadiwa Shilingi milioni 50.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliipongeza Benki ya NMB kwa kuandaa kampeni hiyo, akisema imekuwa kichocheo muhimu kwa jamii katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira na upandaji miti.

Waziri Mchengerwa aliwataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala kote nchini kuhakikisha kila halmashauri inatekeleza agizo la Makamu wa Rais la kupanda miti milioni 1.5 kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhifadhi mazingira.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Ndg. Juma Kimori, alisema benki hiyo imetambua kwa vitendo umuhimu wa mazingira na iliahidi kupanda miti milioni 1, lakini imevuka lengo hilo kwa kupanda miti milioni 1.4.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu nchini, Prof. Dos Santos Silayo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu kutoka TFS, Bw. Hamza Katete, alisema mahitaji ya bidhaa kutoka kwenye rasilimali za misitu nchini ni zaidi ya mita za ujazo milioni 62.3 kwa mwaka, huku uwezo wa misitu iliyopo kuzalisha ukiwa ni mita za ujazo milioni 42.8 pekee—hali inayoonesha pengo kubwa linalopaswa kuzibwa kupitia juhudi za upandaji miti.

Mbali na Shule ya Mwambisi Forest kuibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia Sh milioni 50, Shule ya Msingi Ibondo kutoka Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza ilishika nafasi ya pili na kuzawadiwa Sh milioni 30, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Shule ya Sekondari Itimba ya Wilaya ya Mafinga, mkoani Iringa ambayo ilizawadiwa Sh milioni 20.







Post a Comment

0 Comments