Na Mwandishi Wetu, Kilwa
Katika kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira, Shirika la Bengo kupitia Mradi wa Matumizi Endelevu ya Mikoko, limekabidhi rasmi boti yenye thamani ya Shilingi milioni 67 pamoja na vifaa vya urejeshaji wa mikoko kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na vikundi vya uhifadhi vya kijamii katika Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.
Tukio hilo muhimu lilifanyika Aprili 11, 2025 na kuongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa (DAS), Yusuph Mwinyi, likihudhuriwa na zaidi ya wanajamii 150 kutoka maeneo mbalimbali ya Kilwa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, DAS Mwinyi alilipongeza shirika la WWF pamoja na TFS kwa juhudi zao madhubuti katika kulinda na kuhifadhi mazingira, akisisitiza kuwa jitihada hizo zinaendana na vipaumbele vya kitaifa na kimataifa katika masuala ya uhifadhi.
Aidha, alitoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na mashirika hayo kwa dhati katika kulinda mikoko ambayo ni nguzo muhimu katika mfumo wa ikolojia ya pwani.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa WWF nchini, Almas Kashindye alieleza kuwa shirika hilo linaendelea kujidhatiti katika kulinda rasilimali za baharini, huku mikoko ikiwa moja ya maeneo ya kipaumbele katika ajenda ya uhifadhi endelevu.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Msaidizi wa Meneja wa Usimamizi wa Rasilimali za Misitu na Nyuki – Kanda ya Kusini, Bw. Reginald Lyimo alishukuru kwa msaada huo, akibainisha kuwa boti na vifaa vilivyotolewa vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa shughuli za ulinzi na urejeshaji wa mikoko.
Naye Valeli Bugota, Kiongozi wa Mradi wa WWF, alieleza kuwa mradi huo umejengwa kwa msingi wa ushirikishwaji wa jamii, lengo kuu likiwa ni kuimarisha umiliki wa rasilimali na uwajibikaji wa pamoja katika utunzaji wa mazingira.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa tukio la upandaji wa miche ya mikoko, ambapo DAS Mwinyi aliongoza wananchi katika uzinduzi rasmi wa kampeni ya urejeshaji wa mikoko katika maeneo yaliyoharibiwa.
0 Comments