Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza kuwa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu itatolewa Aprili 13, 2025, katika ukumbi wa The Superdome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 7, Prof. Mkenda amesema kuwa tuzo hizi zinalenga kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, kukuza Lugha ya Kiswahili, na kuongeza ufanisi katika matumizi ya Kiswahili, pamoja na kuhifadhi historia, tamaduni, na maadili ya nchi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema kuwa utoaji wa tuzo hizi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022 umeendelea kuwa na mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuinua waandishi bunifu wa Tanzania.
Mwenyekiti wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Prof. Penina Mlama, ameeleza kuwa tuzo hizo zimewaniwa katika vipengele vinne: waandishi wa riwaya, waandishi wa mkusanyiko wa mashairi au tenzi, hadithi za watoto, na tamthiliya. Ametaja zawadi kwa washindi, ambapo mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 10, ngao, cheti, na kuchapishiwa kitabu chake; mshindi wa pili atapata shilingi milioni saba na cheti; na mshindi wa tatu atapata shilingi milioni tano na cheti.
Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Uandishi Bunifu ya Mwalimu Nyerere mwaka huu.
0 Comments