Na mwandishi wetu
Serikali imesema kuwa moja ya sababu za udumavu wa watoto katika baadhi ya mikoa nchini ni tabia ya ulaji wa chakula cha aina moja, licha ya mikoa hiyo kuongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Sylvia Sigula, aliyetaka kujua sababu za viwango vya juu vya udumavu katika mikoa ya Iringa, Ruvuma, Rukwa na Katavi.
"Ni kweli mikoa hii inaongoza kwa uzalishaji wa chakula lakini asilimia tisa ya watu wanakula chakula mchanganyiko, maana yake asilimia nyingine yote wanakula cha aina moja mfano mtu anaweza kutengeneza makande yakaliwa kwa muda mrefu kidogo badala ya kula chakula kingine,” amesema Dk Mollel.
Amebainisha kuwa katika maeneo hayo, hali ya lishe bado siyo ya kuridhisha kwani udumavu huanza kipindi cha ujauzito ambapo mjamzito anakosa lishe bora, hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka mitano.
Dk. Mollel ameongeza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali, inaendelea kutekeleza mikakati ya kuhamasisha lishe bora na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kula chakula mchanganyiko kama njia ya kupambana na udumavu nchini.
0 Comments