Na mwandishi wetu
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa Kipupwe wa Juni hadi Agosti (JJA) 2025, ikieleza kuwa kipindi hicho kitatawaliwa na baridi kali, upepo mkali na vipindi vya mvua nje ya msimu katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema kuwa maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi kali, huku upepo kutoka Kusini Mashariki ukitawala sehemu nyingi. Alieleza kuwa vipindi vya upepo mkali zaidi vinatarajiwa hasa katika ukanda wa Pwani na baadhi ya maeneo ya nchi kavu, hasa katika miezi ya Juni na Julai.
BARIDI KALI KUSINI NA MAGHARIBI
Katika maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi kama Rukwa, Njombe, Iringa, na Songwe, kiwango cha joto kinatarajiwa kushuka hadi nyuzi joto 6°C au chini ya hapo, huku maeneo ya miinuko yakitarajiwa kuwa na baridi zaidi. Aidha, baridi kali inatarajiwa pia katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Rukwa, na magharibi mwa Dodoma, hasa mwezi Julai.
MVUA NJE YA MSIMU ZATARAJIWA KATIKA MAENEO MACHACHE
Ingawa kipindi cha JJA huwa na ukavu wa kawaida, vipindi vya mvua nje ya msimu vinatarajiwa kujitokeza katika ukanda wa Ziwa Victoria ikiwemo mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Mara, Simiyu na Shinyanga. Vipindi vya mvua pia vinaweza kujitokeza katika mikoa ya Pwani ya Bahari ya Hindi kama Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Lindi, Mtwara, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
MIFUMO YA KIMATAIFA KUATHIRI HALI YA HEWA
Dkt. Chang’a alisema kuwa hali ya joto katika Bahari ya Pasifiki ya tropiki ya kati inatarajiwa kuwa ya wastani, huku joto la juu ya wastani likitarajiwa mashariki mwa Bahari ya Hindi, eneo la karibu na Indonesia. Aidha, joto la juu ya wastani kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi linatarajiwa kupunguza kasi ya upepo baridi kutoka kusini na hivyo kuathiri mwelekeo wa hali ya baridi kwa kiasi fulani.
ATHARI ZINAZOWEZA KUJITOKEZA
TMA imeonya kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa magonjwa yanayohusiana na baridi kama vile homa ya mapafu, pamoja na yale ya mifugo, hasa katika maeneo ya magharibi na nyanda za juu kusini. Aidha, upepo mkali unaweza kuchangia kuibuka kwa vumbi linaloweza kusababisha matatizo ya macho. Pia, hali ya ukavu inatarajiwa kuchangia upungufu wa maji na malisho kwa mifugo.
USHAURI KWA UMMA NA WADAU
Wananchi, hususan watoto, wazee na watu wenye magonjwa sugu, wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya baridi kali. Wafugaji wamehimizwa kuhifadhi malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao. Sekta ya afya imeshauriwa kujiandaa kwa magonjwa yanayoweza kuchochewa na hali ya baridi. Aidha, wadau wa kilimo wanashauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa kwa ukaribu ili kupanga shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
TMA imesisitiza kuwa itaendelea kutoa taarifa za mwelekeo wa hali ya hewa kadri hali inavyoendelea kubadilika, na kuwahimiza wananchi kufuatilia taarifa hizo kupitia vyombo rasmi vya habari na mitandao ya kijamii ya mamlaka hiyo
0 Comments