LUKUVI AIPONGEZA WIZARA YA NISHATI KUTEKELEZA AZMA YA SERIKALI YA KUHAMIA KATIKA MJI WA SERIKALI MTUMBA

 


Na mwandishi wetu

📌 *Aishukuru Wizara kwa kumheshimisha Dkt.Samia Suluhu Hassan*


📌 *Ampongeza Dkt. Biteko kwa kuweka msukumo wa Watumishi kuhamia Mtumba*

Wizara ya Nishati imepongezwa kwa kuhamia rasmi katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambapo Idara na Vitengo vyote vya Wizara sasa vimeshahamia katika jengo la Wizara lililopo katika Mji huo wa Serikali.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge  na Uratibu, Mhe. William Lukuvi wakati alipotembelea jengo la Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba ambapo alipokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. James Mataragio pamoja na Menejimenti ya Wizara.

"Nakupongeza sana  Katibu Mkuu kwa hatua hii, pamoja na Mkandarasi wa Jengo  na Msimamizi, pia nawapongeza kwa nia thabiti ya kuhamia katika Mji huu wa Serikali baada ya Mhe. Rais Samia kutoa fedha zilizowezesha ujenzi wa majengo haya Serikali Mtumba".  Amesema Mhe. Lukuvi

Ameongeza kuwa, nia ya Rais,  Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa ufanisi  katika eneo moja na hivyo kuondoa usumbufu wa kutumia muda mrefu kupata huduma katika maeneo tofauti.

‘ Nawashukuru sana Wizara kwa kumheshimisha Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu nia yake ni Watumishi kuwa pamoja katika utoaji wa huduma ili kuleta ufanisi.” Amesema Mhe. Lukuvi

Amempongeza pia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa kuweka msukumo kwa Wizara katika kukamilisha jengo hilo na kwa watumishi kuhamia katika jengo husika.

Aidha Mhe. Lukuvi ametoa rai kwa watumishi wa Wizara kuhakikisha wanatunza vyema miundombinu na vifaa vilivyopo ili viweze kudumu kama ilivyokusudiwa.






Post a Comment

0 Comments