Na mwandishi wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amezindua PROJECT AMINI iliyo chini ya Bright Africans inayolenga kuwaandaa vijana kwa maisha baada ya masomo kwa kuwajengea stadi za maisha, ujuzi wa ushindani katika soko la ajira na uwezo wa kuleta mageuzi Chanya ya kiuchumi kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Julai 27, 2025 Mhe. Ridhiwani amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetekeleza mikakati thabiti ya kuwawezesha vijana kushiriki kimakimilifu katika maendeleo ya Taifa kijamii na kiuchumi
Amesema kuwa serikali imetengeneza mazingira bora kwa vijana kwa kuandaa mipango na programu mbalimbali zinazohusu maendeleo ya vijana ikiwemo programu ya Taifa ya kukuza Ujuzi ambayo inasaidia kutoa ujuzi kwa vijana kwa nadharia na vitendo, programu ya Uanagenzi na Mikopo kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Aidha Mhe. Ridhiwani ametoa wito kwa vijana kuendelea kutumia fursa kwa bidiii zinazotolewa na serikali Pamoja na wadau, huku akisisitiza sekta binafsi, taasisi za elimu, mashirika ya kiraia na washiriki wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali katika kuunga mkono juhudi za kuwainua vijana.
0 Comments