Waziri Kombo aagana na Balozi wa Slovakia

 





Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amekutana na kuagana na Balozi wa Jamhuri ya Slovakia, Mhe. Katarína Žuffa Leligdonová, ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini .

Mhe. Waziri Kombo ameagana na Mhe. Balozi Katarína Žuffa Leligdonová katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam 

Akizungumza wakati wa mazungumzo na kuagana, Mhe. Kombo amemshukuru Mhe. Balozi Leligdonová kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Slovakia na kunmtakia mafanikio mema katika majukumu yake yajayo.

Mhe. Kombo amesema ushirikiano unaoendelea kukua kati ya Tanzania na Slovakia katika sekta za elimu, kilimo, nishati mbadala, umewezesha kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.

“Kuna nafasi zaidi ya kuongeza maeneo ya ushirikiano kati ya Slovakia na Tanzania hasa katika sekta ya utalii, madini, usafiri wa umma, biashara ya malori, kilimo na matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika kuleta maendeleo ya wananchi wa pande zote na kukuza uchumi” alisema Mhe. Kombo.

Mhe. Kombo pia aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Slovakia kwa kukamilisha taratibu zote za awali za kufungua Ubalozi wake wa kwanza nchini na kusema kuwa hatua inaashiria kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili.

Kwa upande wake, Mhe.Balozi Leligdonová ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano alioupata katika utekelezaji wa majukumu yake, na amesisitiza kuwa uzoefu wa Slovakia katika teknolojia ya kisasa ya utengenezaji wa bidhaa, kilimo, na usindikaji wa viwandani; unatoa fursa ya kuimarisha uhusiano wa watu kwa watu na kukuza diplomasia ya maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.



Post a Comment

0 Comments