Na mwandishi wetu
Mamlaka ya Vipimo nchini (WMA) imewataka wananchi kuhakikisha wanajiridhisha na usahihi wa vipimo vinavyotumika wakati wa kununua bidhaa na kupata huduma mbalimbali, ili kujilinda dhidi ya udanganyifu unaoweza kufanywa na baadhi ya wauzaji wasio waaminifu.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Afisa kutoka WMA Veronica simba alisema kuwa lengo la mamlaka hiyo ni kuhakikisha haki ya mlaji inalindwa kwa kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara mbalimbali ni sahihi na vinazingatia sheria na viwango vilivyowekwa.
"Ni muhimu kwa wananchi kuwa na tabia ya kuangalia na kuuliza kuhusu usahihi wa vipimo kabla ya kulipa. Wapo baadhi ya wafanyabiashara wanaobadilisha au kutumia mizani isiyo sahihi kwa makusudi ili kupata faida isiyo halali," alieleza Afisa huyo.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa wananchi wana haki ya kupewa huduma kwa vipimo sahihi na kwamba wanaweza kutoa taarifa kwa WMA endapo watabaini udanganyifu wowote. Aidha, WMA imeendelea na zoezi la ukaguzi wa mara kwa mara kwa wauzaji katika masoko, maduka na maeneo ya huduma ili kuhakikisha vipimo vinavyotumika vina leseni na vimehakikiwa.
Katika banda la WMA kwenye maonesho hayo, wananchi wamekuwa wakielimishwa kuhusu namna ya kutambua mizani au vipimo vilivyohakikiwa pamoja na umuhimu wa kushirikiana na mamlaka hiyo katika kulinda haki zao.
WMA pia imewahamasisha wafanyabiashara kuhakikisha wanatumia vipimo vilivyohakikiwa kisheria na kutambua kuwa ni kosa la jinai kutumia vipimo visivyofaa au kujaribu kudanganya wateja.
Kwa ujumla, Mamlaka ya Vipimo imesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi, wafanyabiashara na mamlaka hiyo ni muhimu katika kujenga mazingira ya haki na uaminifu katika biashara nchini.
0 Comments