DED KONDOA AKOSHWA NA OUT MAONESHO YA NANENANE - DODOMA

 


Na mwandishi wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Ndg. Shaban Millao, amekipongeza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kutoa elimu bora kwa gharama nafuu, pamoja na kuwezesha watumishi wa umma kuendelea na masomo bila kuathiri utendaji wao wa kazi.

Ndg. Millao. ameyasema alipotembelea banda la OUT kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema kwamba OUT imekuwa mkombozi kwa watumishi na wananchi wa kawaida waliokuwa na ndoto ya kujiendeleza kielimu lakini walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya muda na gharama kubwa za masomo.

“Sina mashaka na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa kutoa elimu bora, na kutoa fursa kwa watumishi kusoma wakiwa kazini. Hii ni hatua kubwa sana kwa maendeleo ya elimu nchini, ongezeni katika kukikatangaza chuo ili wananchi waweze kuwafahamu zaidi na kuwatofautisha na wengine,” amesema Ndg. Millao.

Aidha, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Chuo Dkt. Adam Namamba, amesema kuwa asilimia 60 ya wanafunzi wa shahada ya kwanza katika chuo hicho wanahitimu masomo yao ndani ya kipindi cha miaka mitatu, jambo linalodhihirisha ufanisi wa mfumo wa elimu kwa masafa unaotumika OUT.

Akizungumza katika Maonesho hayo Dkt. Namamba, amesema mafanikio hayo yanatokana na mazingira wezeshi ya ujifunzaji kwa njia ya kidijitali, yanayowawezesha wanafunzi kujifunza bila ya vikwazo vya kimazingira.

“Kwenye shahada ya kwanza tumeweka muda wa miaka mitatu mpaka sita lakini asilimia 60 ya wanafunzi wanahitimu ndani ya miaka mitatu. Hii ni ishara tosha kuwa mfumo wetu wa elimu unafanya kazi kwa ufanisi mkubwa,” amesema Dkt. Namamba.

Ameongeza kuwa kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET), unakwenda kusaidia kuleta uwiano wa wasomi wa sayansi kwa kuongeza udahili katika programu za kisayansi, kuimarisha miundombinu, na kuhamasisha ushirikiano na sekta za viwanda na biashara.

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimeendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na wadau wanaotembelea banda la chuo hiki katika viwanja vya Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma, kwa lengo la kueleza fursa mbalimbali zinazotolewa  na chuo hiki.

Post a Comment

0 Comments