RAIS MWINYI ATEMBELEA ENEO LA OFISI ZA MJI WA SERIKALI NA LINALOJENGWA UWANJA MPYA WA AFCON

 



Na mwandishi wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi mkubwa wa uwanja wa AFCON pamoja na miundombinu mbalimbali inayojengwa Fumba, hivyo ni muhimu kubaini mapema maeneo yatakayotumika kwa mradi huo ili kuepusha mwingiliano wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo kati ya taasisi husika.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Ikulu Zanzibar, tarehe 11 Agosti 2025, katika kikao maalum na mawaziri mbalimbali akiwemo Mhe. Rahma Kassim Ali, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Mhe. Shariff Ali Shariff, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Tabia Maulid Mwita, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, pamoja na Taasisi ya Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (ZPDB), kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja kuhusu matumizi sahihi ya ardhi katika maeneo ya uwekezaji Fumba.

Mara baada ya kikao hicho, Rais Dkt. Mwinyi aliridhia mapendekezo yaliyoafikiwa katika kikao hicho ya kutembelea maeneo husika ya Fumba, ili kupata uhalisia wa miradi hiyo pamoja na mtandao wa barabara, hatua itakayosaidia kupanga utekelezaji kwa ufanisi na kuondoa changamoto za upangaji wa ardhi. Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi pia alitembelea eneo linaloendelea kujengwa viwanja vya michezo vitakavyotumika kwa michuano ya AFCON 2027.

Akihitimisha ziara yake, Rais Dkt. Mwinyi alipata fursa ya kuzungumza na wakaazi wa Kisakasaka ambao wametoa maeneo yao kupisha ujenzi wa Ofisi za Serikali na jengo la Baraza la Wawakilishi. Amewahakikishia kuwa Serikali itawafidia ardhi zao kwa fedha au nyumba za makaazi, kulingana na ridhaa ya kila mmoja.























Post a Comment

0 Comments