Nungwi, Kaskazini Unguja – 18 Septemba 2025
Mgombea wa kiti cha Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameungana na Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Michezo Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika mkutano huo ulioshuhudiwa na maelfu ya wananchi, Dkt. Mwinyi aliwataka Wazanzibari kuendelea kuiamini na kuiunga mkono CCM, akisisitiza kuwa chama hicho kimeendelea kuwa nguzo ya amani, mshikamano na maendeleo endelevu kwa Taifa la Tanzania, ikiwemo Zanzibar.
Aidha, alibainisha kuwa uongozi wa CCM umekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo sekta za elimu, afya, kilimo, uvuvi na utalii ambazo zimekuwa chachu ya maendeleo na ustawi wa wananchi.
Kwa upande mwingine, mkutano huo pia ulikuwa fursa kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kuinadi Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030, ambapo alieleza mikakati ya serikali ijayo katika kukuza uchumi, kuimarisha huduma za kijamii na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati nchini.
Wananchi wa Nungwi na maeneo ya jirani walijitokeza kwa wingi, wakionesha hamasa kubwa ya kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao na kuonesha imani yao kwa wagombea wa CCM.
0 Comments